Habari Mseto

'Wasichana 160 hupatikana na Ukimwi kila mwaka Murang'a'

August 24th, 2020 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

TAKRIBAN wasichana 160 wadogo kati ya wote 4,000 ambao husaka huduma za utunzaji mimba – antenatal care – katika hospitali kuu ya Murang’a kila mwaka hupatikana na virusi vya ugonjwa wa Ukimwi.

Haya yalifichuliwa na Waziri wa Afya wa Kaunti hiyo, Joseph Mbai aliyeongeza kuwa kati ya wote 16,000 ambao huishi na Ukimwi kaunti hiyo 4,000 ni wa umri wa miaka 18 na kuteremka.

Bw Mbai alisema kuwa wale ambao hupatikana wakiwa wameambukizwa huwekwa katika ratiba ya utumizi wa dawa za kupambana na makali ya HIV (ARVs) na kisha kutunzwa wasiambukize mtoto akiwa bado katika tumbo la mamake.

Aidha, huwekwa chini ya usimamizi wa wahudumu wa afya wa kijamii ambao huhakikisha wanatumia dawa hizo za ARV kama maagizo yasemavyo na pia kuhakikisha wanaendelea kutimiza ratiba ya kliniki kuhusu ujauzito.

Bw Mbai alisema kuwa tawimu hizi hazina ule uhalisia wa kina kwa kuwa zinazingatia tu utafiti ambao umefanywa katika hospitali kuu ya Murang’a huku kukiwa na vituo vingine vya kiafya ambavyo pia takwimu zake zinakusanywa pamoja.

Alisema kuwa takwimu alizoachilia zinazingatia kipindi cha kati ya 2013 na 2019.

Bw Mbai alisema kuwa hali hii ni ya kuzua changamoto kwa wadau na wawajibikie kusaka maafikiano kama ni vyema kuzinduliwe elimu kuhusu madhara ya ngono miongoni mwa walio na umri mchanga.

Mwenyekiti wa maendeleo ya wanawake katika Kaunti hiyo Bi Lucy Nyambura alisema kuwa takwimu hizo zinaangazia jinsi umasikini hudharauliwa na kutumiwa kutendea wengine unyama.

“Utafiti wetu ni kwamba visa hivyo vya mimba za mapema na pia maambukizi ya Ukimwi miongoni mwa wasichana hao wachanga huwa na asilimia 95 ya wazawa ndani ya umasikini,”akasema.

Alisema kuwa walio na ushawishi au pesa katika jamii huwavutia wasichana wachanga kwa vitisho au kwa hela hadi kuwatunga mimba na hatimaye kufunika ukweli kupitia aidha kutoa vitisho au kulipa fidia ya pesa nane kwa familia za waathiriwa.

Alisema kuwa janga kuu katika maambukizi haya ya Ukimwi kwa wasichana wachanga ni kwamba “wao hawafichui hali zao kwa kuwa hata hawajui kabla ya kushika mimba na kujitokeza katika kliniki ambapo ni lazima wapimwe wajulikane hali zao.”

Alisema kuwa kabla ya kupimwa, huwa wanaendelea kushiriki ngono bila kinga na kueneza maambukizi hadi kwa familia za walio katika ndoa “kwa kuwa wengi wa walio na ujambazi wa ngono na wasichana wachanga huwa ni wanaume walio na mabibi nyumbani.”

Mbunge wa Maragua Bi Mary wa Maua alisema kuwa wakati umefika wazazi washinikizwe wachukulie suala la malezi na ushauri kuhusu ngono kwa wayoto wao kama la dharura, wachungaji nao waombee shetani wa ngono na watoto wachanga atokomee huku nayo serikali iwajibikie suala la kuandama wahaini wa kunyanyasa watoto kupitia ngono kwa ukali wote wa kisheria.