Wasichana 330,000 walipata mimba 2020 – Ripoti

Wasichana 330,000 walipata mimba 2020 – Ripoti

Na MORAA OBIRIA

MATINEJA chipukizi zaidi ya 330,000 wenye umri kati ya miaka 10-19 walipachikwa mimba 2020, wakati ambapo wanafunzi walikaa nje ya shule kwa karibu miezi 10.

Ripoti ya Economic Survey 2021 iliyotolewa wiki iliyopita na iliyokusanya data ya wasichana wajawazito kupitia ziara zao za kwanza katika Kliniki za Kina mama Wajawazito (ANC), inaonyesha vijana wengi zaidi chipukizi walipachikwa mimba 2019 kuliko mwakia uliopita.

Utafiti huo uliofanywa na Shirika linaloshughulikia Takwimu Nchini (KNBS) uliashiria kuwa jumla ya wasichana 396,929 walikuwa na mimba 2019.

Mnamo 2020, idadi hiyo ilipungua hadi 332,208, huku wanaharakati wanaopambana kuzuia mimba za mapema wakihoji kuwa haiashirii uhalisia uliopo mashinani.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, 2018 ilijitokeza kama mwaka mbaya zaidi ambapo wasichana 427,297 waligeuzwa wazazi.

Tangu 2016 ambapo visa 275,633 viliripotiwa, idadi hiyo imekuwa ikiongezeka na haijawahi kupungua kamwe, hali inayoibua wasiwasi.

Idadi hiyo ilipanda hadi 339,676 katika mwaka uliofuata kabla ya kufikia zaidi ya 400,000 2018 kisha 2019, ikapungua kwa 30,368.

Wanaharakati wanahoji kuwa asilimia zaidi ya 30 ya visa vya mimba miongoni mwa vijana chipukizi huenda haijajumuishwa kwa sababu vijana chipukizi huogopa kwenda hospitalini kutokana na aibu na unyanyapaa.

Kando na ndoa za watoto, wasichana hupachikwa mimba kupitia kujamiiana baina ya jamaa wa familia na kudhulumiwa kingono kunakowaacha na makovu kisaikolojia na kuvuruga hali ya kujidhamini nafsi.

Kulingana na data kutoka kwa laini ya simu inayotumika kuwasilisha malalamishi ya kijinsia nchini, 1195, kina baba hutekeleza asilimia 37 ya visa vya kushiriki ngono na jamaa wa familia zao, hasa kwa kuwavizia wasichana nyumbani kwao.

Bi Evarlyne Ketukei, mfanyakazi wa afya kwa jamii katika Kaunti ya Kajiado, anasema miongoni mwa wasichana 100 wajawazito, ni 70 pekee wanaohudhuria ANC.

“Huwa wanajifungulia nyumbani na kuja hospitalini tu wakati kuna matatizo au kwa sababu ya chanjo,” anasema.

Bi Emmanuel Kiprotich, anayetetea usawa wa kijinsia katika Kaunti ya Narok chini ya Shirika la Kimataifa kuhusu Vijana na Upangaji Uzazi, anasema hatua ya kufunga makanisa, yaliyokuwa vituo vya kueneza uhamasishaji, ilitatiza juhudi za kuzuia mimba za mapema.

“Kila unapogeuka, utaona msichana mwenye mimba. Haikuwa hivyo 2019. Idadi hiyo ni lazima iwe juu zaidi kuliko 2020. Kwa mfano, binti wawili wa jirani yangu walio katika sekondari walitungwa mimba,”

“Inahuzunisha kwamba wazazi wengi huwa hawajishughulishi kuwapeleka hospitalini kwa ukaguzi. Huwa wanawaacha kutunza mimba zao pekee yao,’ anasema.

Anapendekeza haja ya kuwahamasisha wazazi kuwafunza wavulana na binti zao kuhusu ngono.

You can share this post!

Raila kuhudhuria uzinduzi wa chama cha PAA

Suluhu aashiria kugombea kiti cha urais mwaka 2025