Wasichana wakeketwa na kuozwa Baringo

Wasichana wakeketwa na kuozwa Baringo

Na FLORAH KOECH

LICHA ya serikali kuendelea na mipango ya kufungua upya shule mwezi Januari, kuna hofu ya wanafunzi wengi wasichana kuacha shule katika Kaunti Ndogo ya Tiaty, Kaunti ya Baringo, baada ya wengi wao kukeketwa na kuozwa.

Shule katika eneo hili zimekuwa zikitumiwa kama vituo vya kuwasaidia wasichana wanaotoroka makwao, baada ya kulazimishwa kushiriki kwenye utamaduni huo na wazazi wao.

Wasichana wengi walilazimika kupashwa tohara, baada ya kusalia nyumbani kwa muda mrefu kutokana na janga la virusi vya corona.Wengi waliojipata katika hali hii ni wale ambao bado wako katika shule za msingi walio kati ya umri wa miaka tisa na 17.

Kwa mujibu wa Bi Lilian Chepchumba, ambaye ni mwanaharakati wa kukabili ukeketaji, baadhi ya sababu ambazo zimechangia wasichana wengi kujipata katika hali hiyo ni likizo ndefu kutokana na corona, hali mbaya ya barabara na mawasiliano.

Baadhi ya vijiji viko katika maeneo ya mbali sana, ambayo hayana huduma nzuri za mawasiliano.Alisema maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni Akoret, Tirioko na Silale.

Alieleza kuwa wasichana wengi washapashwa tohara na kuozwa na sasa wengi wao ni wajawazito.Bi Chepchumba alieleza kwamba wakati corona ilipotokea, wasichana ambao walikuwa wametoroka kuepuka utamaduni huo walipashwa tohara kwa nguvu. Hii ni kwa sababu walikuwa wakiishi na watu waliofichua walikokuwa, kwani wengi wao ni marafiki wa wazazi wao.

“Wakati masomo yalikuwa yakiendelea kama kawaida, wasichana wengi walikuwa salama kuliko kuwa nyumbani. Ilikuwa rahisi kwetu kufuatilia waliko. Tungeweza kuwauliza wazazi wao. Ni vigumu sasa kwani wengi wao wako na wazazi majumbani mwao, ambapo huwapa maagizo kuhusu lolote wanalotaka,” akasema.

Masomo

“Shule zilipofungwa Machi, wasichana wengi katika vijiji vilivyo katika maeneo ya mbali walipashwa tohara na kuozwa. Tunahofu kwamba baada ya shule kufunguliwa upya mnamo Januari, huenda wengi wao wakakosa kurejelea masomo yao kabisa,” akasema.

Wazazi wengi katika eneo hilo hawana elimu. Kumekuwa na uvumi vijijini kwamba wanafunzi hawatarejelea masomo yao tena, hali inayotajwa kuwafanya wazazi wengi kuwalazimu wanao kushiriki kwenye ukeketwaji.

Mwanaharakati huyo alisema kwamba wakeketaji wanafahamu utamaduni huo ni kinyume cha sheria, ila wengi wao wamebadili mbinu ili kutotambulika kwa urahisi na maafisa wa serikali.

Alisema wazazi wengi wanawasafirisha wanao kuenda katika kaunti jirani ili kukwepa kukabiliwa kisheria.“Baadhi ya wazazi ambao wanahofia kukamatwa wamebuni mbinu za kuwakwepa maafisa wa serikali. Wanapanga njama wasichana wao wawatembelee jamaa zao katika kaunti jirani ya Pokot Magharibi ambako wanafanyiwa vitendo hivyo,” akasema.

You can share this post!

KDF wavamia kambi ya Al Shabaab msituni Boni, waua wanne

Nauli yapanda Wakenya wakirejea mijini