Habari Mseto

Wasichana waliopachikwa mimba kurejeshwa shuleni

May 11th, 2024 1 min read

WINNIE ATIENO

MBUNGE Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Mombasa Zamzam Mohammed ameapa kuwarejesha wasichana wote ambao walipachikwa mimba na kuacha masomo kabla ya kumaliza mtihani wa Kidato cha Nne.

Kwa jumla Bi Mohammed amerejesha wasichana 350 shuleni kumaliza masomo yao.

Aliwasihi wasichana kutoka kaunti hiyo ambao walisitisha masomo yao baada ya kupachikwa mimba, kurudi shuleni kutimiza ndoto zao.

“Ninawapatia wasichana waliopachikwa mimba na kulazimika kuwa wazazi wakiwa watoto nafasi nyingine ya kutimiza masomo yao. Kwa jumla nimerejesha wasichana 350. Ninawalipia karo ya shule hadi Kidato cha Nne,” alisema Bi Mohammed.

Akiongea kwenye hafla ya kufuzu kwa mahafala wapatao 175 wa chuo anuai cha St Mulumba huko Mikindani, Bi Mohammed aliwatia nguvu wasichana kutokata tamaa licha ya changamoto wanazokumbana nazo.

“Njooni ofisini kwangu niwasaidie,” alisema mwanasiasa huyo.

Mbunge wa Jomvu aliwasihi wasichana kusomea kozi za kiufundi akisema kuna nafasi nyingi za kazi hata ughaibuni.