Wasimamizi waelezea hatua ilizopiga MKU katika utoaji mafunzo ya chuoni

Wasimamizi waelezea hatua ilizopiga MKU katika utoaji mafunzo ya chuoni

Na LAWRENCE ONGARO

WAHITIMU wapatao 5,000 wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) wamehimizwa kuonyesha ujuzi wao baada ya kukamilisha masomo yao.

Katibu katika Wizara ya Elimu anayehusika na Elimu ya Juu na Utafiti Balozi Simon Nabukwesi alipongeza juhudi zinazofanywa na MKU kwa kuzingatia maswala ya utafiti na ubunifu.

Katibu huyo ambaye alikuwa mgeni wa heshima kwenye hafla ya Ijumaa – awamu ya 20 ya kufuzu – alipongeza juhudi zinazoendeshwa na chuo hicho.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wahitimu wachache kwa sababu iliendeshwa kwa mseto ikiwemo kupitia mtandaoni.

MKU ilizingatia sheria za Wizara ya Afya kuhusu kuzuia usambazaji wa Covid-19.

Katibu huyo alipongeza MKU kwa kufanya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Makerere katika maswala ya fedha za utafiti takribani Sh10 milioni tangu mwaka wa 2018.

Alieleza heshima aliyopewa Rais mstaafu Mwai Kibaki kwamba ni jambo la kupongezwa na nchi mbili, Kenya na Uganda, ikizingatiwa aliwahi kusomea katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda.

Mwanzilishi wa MKU Profesa Simon Gicharu, alieleza jinsi chuo hicho kinavyopania kujenga jumba la kisasa la matibabu ambalo litakuwa na makazi ya wanafunzi, jumba la masomo, na maabara ya kipekee.

Alieleza jinsi MKU ilivyotumia takribani Sh300 milioni kujenga chumba cha upasuaji wa maiti cha General Kago katika hospitali ya Thika Level Five.

Prof Gicharu alijitolea kufadhili masomo ya mwanafunzi Milly Nafula ambaye alikosa kujiunga na chuo kikuu miaka 14 iliyopita licha ya kupata alama ya A- katika mtihani wa kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE).

Baada ya masaibu ya mwanafunzi huyo kuangazia katika vyombo vya habari aliamua kuchukua jukumu hilo hadi akamilishe masomo yake.

Chansela wa MKU Prof John Strutters aliyesoma hotuba yake kupitia mtandao akiwa Scotland, alipongeza chuo hicho kwa kuendesha kongamano muhimu la Yunus Global Social Business Summit, mwezi Novemba 2021.

Alieleza kuwa ushirikiano ndio njia ya pekee ambayo itaipa MKU mwongozo wake wa miaka 10 ijayo.

Wakati wa hafla hiyo MKU ilijivunia kupata wahitimu sita ambao wamepiga hatua katika masomo ya uzamifu (pHD) ambapo wawili ni wa jinsia ya kiume nao wanne ni wa jinsia ya kike.

Naibu Chansela Prof Deogratius Jaganyi alipongeza chuo hicho kwa kufunza masomo ya kutambulika kimataifa.

Alisema wanafunzi wengi ni wa kutoka humu nchini lakini pia kuna wa mataifa mengine. Baadhi ya wanafunzi wengine walio katika chuo hicho wanatoka nchi za Nigeria, Burundi, Chad, Gabon, Cameroon na Tanzania.

“Jambo hilo pekee linaashiria umuhimu wa mwenye ari ya kupata elimu kuamua kujiunga na MKU,” alisema Prof Jaganyi.

Alieleza kuwa hivi majuzi chuo hicho kilipata ufadhili wa Sh7 milioni kutoka kwa Shirika la International Research and Development (IRD) kwa lengo la kutoa masomo kuhusu homa hatari ya Covid-19 katika kaunti za Kiambu na Nairobi.

Alipongeza juhudi za chuo hicho kuwafikia wakazi wa mashinani na kuwafadhili na misaada tofauti.

You can share this post!

Raila azindua safari ya ikulu kwa ahadi nyingi

Okutoyi arejea nyumbani baada ya jeraha

T L