Wasimulia jinsi walikaa shimoni siku 7 bila chakula

Wasimulia jinsi walikaa shimoni siku 7 bila chakula

Na ANGELINE OCHIENG

WANAUME watatu waliookolewa na wanakijiji baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka na kuwafunika humo, wameelezea masaibu waliyopitia kuishi shimoni bila chakula kwa siku saba katika eneo la Abimbo, Bondo, Kaunti ya Siaya.

Philip Joel Ogutu, 21, Victor Otieno, 20, na Jacob Onyango, 23, walitaja kuokolewa kwao kama miujiza.Watatu hao walikuwa miongoni mwa wachimba dhahabu 10 waliofunikwa na mchanga Alhamisi iliyopita.Watatu hao waliokolewa jana alfajiri na kufikisha idadi ya manusura hadi watu wanane.

Mmoja alitolewa kwenye shimo hilo akiwa amefariki Jumamosi na mwingine hajulikani aliko.Philip, ambaye amekuwa akifanya kazi ya kucheza muziki (DJ) jijini Kisumu, alienda kijijini Abimbo kuhudhuria mazishi.Kisha akajiunga na wenzake kwa shughuli ya kuchimba mchanga ili kujipa fedha zaidi za kutumia kipindi hiki cha sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Watatu hao walieleza kuwa wakiwa humo shimoni hawakuweza kutofautisha kati ya mchana na usiku kwani walikuwa wamegubikwa na giza. Waligeukia maombi na nyimbo za kumsifu Mungu huku wakisubiri tu kifo, kabla ya kuokolewa kimuujiza.

“Tulikuwa tunalala na kuamka bila kujua ikiwa ilikuwa mchana au usiku,” akasema Bw Ogutu ambaye alifanya kazi hiyo kwa takribani wiki tatu kabla ya kukumbwa na mkasa huo.“Ni muujiza kwamba tuliishi shimoni kwa siku saba bila kula chakula,” akaongeza Bw Ogutu anayeendelea kupokea tiba katika hospitali ya Bondo pamoja na wenzake wawili.

Taifa Leo ilipowatembelea hospitalini, watatu hao walionekana wachangamfu na wenye nguvu. Hata hivyo, Victor Otieno alikuwa na changamoto ya kupumua kutokana na muda mrefu aliokaa ardhini.Waathiriwa walikuwa wakichimba dhahabu katika shimo la urefu wa futi 150.

Wakiwa humo walisikia mtetemo wa ardhi na hapo ndipo walijua kwamba huo ulikuwa mwisho wao.“Tulikimbia katika ‘mlango’ tuliokuwa tumeingilia tukakuta umefungwa kwa mchanga. Rafiki yangu Onyango alishauri tutulie hadi tutakapookolewa na watu waliokuwa nje,” asimulia Bw Ogutu.

Wachimbaji hao walikuwa wamebeba tochi walizokuwa wakitumia kumulika ndani ya mgodi. Lakini zilizimika baada ya siku mbili na kuwaacha gizani.“Hatukuwa tumebeba chakula na miili yetu ilizidi kudhoofika kila siku. Tulilazimika kunywa maji ya chumvi yaliyo kwenye mgodi ili kurefusha siku za kuishi.

Mkasa huo umenifanya kuwa karibu na Mungu,” alihoji Bw Ogutu.

You can share this post!

Njaa: Mbunge aomba wahisani wawasaidie wakazi na chakula

Wakazi walalamika unyakuzi bandarini

T L