Habari

Wasio na uwezo kusikia kutumia maski spesheli kusoma midomo ya wazungumzaji

May 22nd, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

WALEMAVU wasio na uwezo wa kusikia katika Kaunti ya Mombasa wamepokea maski spesheli kutoka kwa Muungano wa Watu Wanaoishi na Ulemavu Pwani.

Maski hizo zimeundwa kwa vitambaa maalum, lakini vyenye sehemu za kuonyesha midomo ya wazungumzaji kinyume na maski zingine zinazotumika kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Aidha, wamepewa chakula kitakachowafaa pakubwa wakati huu ambapo wakazi wanapitia wakati mgumu kutokana na athari hasi za kiuchumi kufuatia janga la Covid-19.

Bi Hamisa Zaja (kulia) na wanachama wengine wakitoa chakula kiwafae walioathirika vibaya sana kiuchumi na janga la Covid-19 Kaunti ya Mombasa Mei 21, 2020. Picha/ Mishi Gongo

Akizungumza Alhamisi katika hafla iliyofanyika Tudor, muuguzi katika hospitali kuu ya eneo la Pwani Bi Fatma Ngoto ambaye pia anashughulikia lugha ya ishara katika hospitali hiyo, aliwafuwandisha jinsi ya kutumia maski hizo na kudumisha usafi.

“Maski hizi zitawawezesha kuzungumza kati na baina yenu kwa urahisi,” akasema.

Muuguzi huyo alisema kukosa uhamasisho na mafunzo ya kutosha ni changamoto kuu katika vita dhidi ya virusi vya corona.

Afisa mkuu katika muungano huo Bi Hamisa Zaja aliilaumu serikali kwa kuwaacha nyuma katika vita dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.

“Serikali inapaswa kujumuisha watu wanaoishi na ulemavu katika vita hivi. Katika ugavi wa chakula na maski, watu wanaoishi na ulemavu wanafaa kuwekwa katika mstari wa mbele,” akasema.

Bi Hamisa Zaja (kulia) na Bi Fatma Ngoto (kati nyuma) wakipeana maski spesheli kwa wakazi wa Kaunti ya Mombasa. Picha/ Mishi Gongo

Aidha Bi Zaja aliiomba serikali kuleta maski maalum.

Alisema maski zilizoko sokoni kwa sasa haziwafai watu wanaoishi na ulemavu; hasa wasio na uwezo wa kusikia.

“Ni vigumu kutumia lugha ya ishara bila kuona midomo na maski zilizoko sokoni kwa sasa zinaficha midomo hivyo kuwanyima wasio na uwezo wa kusikia fursa ya kuzungumza,” akasema.