Wasio na vyeti vya chanjo kukosa huduma za serikali

Wasio na vyeti vya chanjo kukosa huduma za serikali

Na WAANDISHI WETU

Ripoti za Winnie Onyando, Daniel Ogetta na Elizabeth Merab

WAKENYA ambao hawana cheti cha kupokea chanjo hawataruhusiwa kupokea huduma za serikali ifikapo mwisho wa mwezi huu.

Tangazo hilo linafuata ongezeko la idadi ya maambukizi ya virusi vya corona nchini. Serikali kupitia Wizara ya Afya ilisema kuwa yeyote ambaye hana cheti hicho hataruhusiwa kupata huduma kwenye baa, mikahawa, mikutano mbalimbali, ofisi za serikali, duduma za usafiri na kwenye maduka zilizo na leseni za kazi kutoka serikalini.

Akizungumza na wanahabari, Katibu katika Wizara ya Afya, Mercy Mwangangi, alisema kuwa kanuni hizo ni kuhakikisha kuwa nchi imewachanja watu 10 milioni ifikapo mwisho wa mwezi huu. “Ukiwa hujachanjwa, hutaruhusiwa kupata huduma za kusafiri. Hutaruhusiwa kupanda pikipiki, magari ya umma, gari la maoshi hata ndege. Lazima uonyeshe cheti chako cha chanjo,” akasema Dkt Mwangangi.

Hata hivyo, wale ambao hawajapata chanjo sharti watumie barua inayoeleza sababu za kukosa kuchanjwa kutoka kwa madaktari walio na leseni. Vyeti vya chanjo hata hivyo havipaswi kuhifadhiwa nyumbani, kwani vitatumika kama thibitisho na shahidi kuwa umechanjwa.

Kila kituo au mratibu wa hafla atahitajika kuteua mtu ambaye atapewa jukumu la kuthibitisha vyeti vya chanjo katika sehemu zote nchini. Kadhalika, wafanyikazi na watoa huduma wote katika kila taasisi lazima wawe wamepata chanjo ndipo waruhusiwe kuingia kazini.

Hata hivyo, Dkt Mwangangi alitupilia mbali kauli kuwa chanjo ni ya lazima. Alisema kuwa yeyote ambaye anataka kutangamana na jamii, sharti achanjwe. “Si lazima upate chanjo ila ukitaka kutangamana na watu mbalimbali nchini, lazima uwe umechanjwa na una cheti chako.”

Wale ambao watahudhuria hafla za harusi, kutembelea mbuga mbalimbali pia watahitajika kuwa na cheti chao cha chanjo. “Kila mmoja ambaye amechanjwa atapakua cheti chake kwenye tovuti ya Wizara ya Afya. Anaweza kuchapisha cheti hicho au kukipakua na kukitumia ikiwa kwenye simu ya kisasa,” akasema Dkt Mwangangi.

Kufikia Desemba 21, jumla ya Wakenya 9.2 milioni wamechanjwa. Hii inasukuma idadi ya watu wazima waliopatiwa dozi zote mbili kufika asilimia 13.4. Vijana 13,845 walio na umri kati ya 15 na 18 wamepokea dozi ya kwanza ya chanjo aina ya Pfizer.

Kutoka sampuli 11,197 waliopimwa, watu 3,328 walipatikana na virusi hivyo. Kenya imepokea jumla ya dozi 23 milioni huku chanjo zinazotumika sana nchini zikiwa AstraZeneca/Covishield, Pfizer, Moderna, Sinopharm na Johnson and Johnson. Haya yanajiri wiki moja baada ya kesi kuwasilishwa katika Mahakama Kuu ya kusitisha agizo la Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe kufuatia ombi lililowasilishwa na mfanyabiashara, Enock Aura.

Hata hivyo, Jaji Antony Mrima wiki jana alisema kuwa agizo la Bw Kagwe halipaswi kutekelezwa hadi kuamuliwa kwa kesi hiyo. “Mlalamishi amewasilisha ushuhuda kwamba wale ambao hawatatoa ushahidi juu ya kupokea chanjo watazuiwa kupata huduma muhimu kutoka kwa idara za serikali,” akasema Jaji Mrima.

You can share this post!

Serikali za Uganda, Kenya zakubaliana kusitisha sheria tata...

Zaha kutegemewa na Ivory Coast kwenye AFCON 2022 nchini...

T L