Habari Mseto

Wasiomwamini Mungu waitaka serikali kuwatengea Sikukuu

August 20th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

MUUNGANO wa watu wasioamini uwepo wa Mungu (AIK) sasa unaitaka serikali kutenga siku ya sikukuu yao, namna ilivyoteka sikukuu ya Wakristo na Waislamu.

Kulingana na watu hao wanaopinga imani za kidini, serikali imewabagua, hivyo wakimtaka waziri wa usalama wa ndani Dkt Fred Matiang’i kutenga Februari 17, tarehe ambayo muungano huo ulitambuliwa nchini kuwa sikukuu yao.

Kulingana nao, siku hiyo itawapa fursa kueneza ujumbe kuwa hakuna Mungu katika kila kaunti, namna waumini wa dini hupigia debe dini zao.

“Tunataka siku ambayo tutawadhihirishia kuwa hakuna Mungu ama kiumbe kingine chenye nguvu cha kuabudiwa. Tunataka serikali kuidhinisha Februari 17 kila mwaka kuwa sikukuu ya watu wasiomwamini Mungu,” ikasema habari kutoka kwa AIK, iliyotiwa sahihi na naibu wa rais wa muungano huo, Bi Daisy Siongok.

Muungano huo unarejelea katiba ya kenya inayoelekeza kuwa kila mtu ana uhuru wa kuamini anavyopenda, hivyo wakitaka kutambuliwa na kuheshimiwa kama vikundi vingine vya kidini.

“Tutatumia fursa hiyo kuandaa tamasha za kueneza ujumbe kuwa hakuna Mungu ili kuzidi kuwajulisha watu kuhusu namna ya kutoamini nchini. Tunaamini kuwa hii ni namna moja ya kudhihirisha uhuru wa watu kama inavyosema katiba,” akasema Bi Siongok.