Habari Mseto

Wasiopeleka watoto wao shuleni waonywa

October 18th, 2018 1 min read

Na Fadhili Fredrick

SERIKALI imeonya kuwa itawachukulia hatua kali wazazi na walezi katika kaunti ya Kwale ambao wanawanyima watoto haki ya kupata elimu.

Katika mkutano wa usalama uliofanyika Kinondo juma lililopita na kushirikisha idara ya usalama na kamati za amani na usalama, ilibainika kuwa kuna idadi kubwa ya watoto ambao hawaendi shuleni.

Naibu Kaunti kamishna wa Msambweni, Bw Ronald Enyakasi amewataka wazazi na walezi kuwapeleka shuleni watoto wao, kinyume na hilo alisema watasakwa popote walipo na kuchukuliwa hatua za kisheria.

”Tumewaagiza machifu na manaibu wao kuwatafuta wazazi wasipowapeleka watoto wao shuleni na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kiwanyima watoto wao haki ya kusoma,” aliambia Taifa Leo kwa njia ya simu Jumanne.

Bw Enyakasi alionya kuwa uhalifu huenda ukaongezeka kufutia ongezeko la watoto wasiohudhuria shuleni na hatimaye huenda wakajiunga na makundi ya uhalifu.

Alisema ni katika makundi hayo ambapo watoto hujiingiza katika matumizi mabaya ya madawa ya kulevya wakiwa wadogo na kuharibu maisha yao.

Mwenyekiti wa kamati ya Amani na Usalama katika eneobunge la Matuga Bi Mwanakombo Jarumani alisema kesi za watoto kuacha shule ni nyingi eneo hilo na wengi hujishughulisha na kazi za matimboni.

Bi Jarumani alisema ni jambo la kusikitisha kuona watoto wanafanyakazi kazi matimboni ili hali wanastahili kuwa shuleni.

“Tuna idadi kubwa ya watoto huko Matuga ambao wanafanya kazi matimboni na kujihusisha na uhalifu badala ya kwenda shule,” akasema, akiongeza kwamba jamii inastahili kuangazia jambo hilo haraka iwezekanavyo na kuwapeleka watoto shule.

Alisema wengi ya wale wasiohudhuria shule wanaweza kushirikishwa katika uhalifu.

Naye Mwenyekiti wa Amani na Usalama wa Msambweni Bw Katiba Mkungu aliwahimiza wazazi kuwa mstari wa mbele katika kufundisha watoto wao kwa ajili ya maisha baadaye.

“Tumegundua kwamba baadhi ya watoto wetu hawaendi shuleni na tunahitaji kuamka kama wazazi na kuwapeleka watoto wetu shuleni ili kuwajengea maisha yao ya baadaye,” akasema.