Habari Mseto

Wasiwasi Nyeri visa vya corona vikiongezeka

June 9th, 2020 1 min read

NA IRENE MUGO

Kuongezeka kwa visa vya corona Kaunti ya Nyeri kumezua wasiwasi kati ya maafisa wa afya kaunti hiyo huku wakiwahimiza wananchi kufuata maagizo yaliyowekwa na serikali baada ya watu tisa kupatikana na virusi vya corona.

Akiongea huku akipokea msaada wa Sh500,000 kutoka kwa kampuni ya Britam, Gavana Mutahi Kahiga alisema kwamba kati ya hao tisa ni mmoja pekee aliyeonyesha dalili za corona.

Maafisa wa afya watatu wamesemekana kuugua ugonjwa huo baada ya kumhudumia mgonjwa ambaye hakuwa anaonyesha dalili zozote katika hospitali ya Nyeri.

Watatu hao wametengwa katika hospitali ya Mlima Kenya ambayo ina idadi ya vitanda 15.

Kulingana na Bw Kahiga, kaunti hiyo ilikuwa imejitayarisha kukabiliana na virusi hivyo vya corona. Aliwahakikishia wakazi kwamba kupatwa na ugonjwa wa corona si hukumu ya kifo.