Habari Mseto

Wasiwasi tanki la petroli likifuka moshi usiku katika kituo cha mafuta

April 17th, 2024 1 min read

NA ANTHONY KITIMO

HOFU ilitanda katika eneo la Saba Saba, Kaunti ya Mombasa baada ya mlipuko kutokea Jumanne usiku katika kituo cha kuuza mafuta.

Kulingana na Bw Kevin Mwiti ambaye ni mhudumu katika kituo hicho mafuta cha OLA, mlipuko ulisikika ndani ya tanki la mafuta mwendo wa saa mbili na nusu usiku kisha moshi ukaanza kufuka.

Afisa mkuu katika idara ya kupambana na majanga ya moto Kaunti ya Mombasa, Bw Ibrahim Basafar, alisema tatizo hilo lilisababishwa na moja ya nyaya za stima katika tanki hilo lakini waliweza kudhibiti kutokea kwa moto.

Wataalamu kutoka idara ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA) tayari wamezuru eneo hilo kwa uchunguzi zaidi.

Mkuu wa polisi wa Mombasa Maxwell Agoro alisema waliweza kuarifu wakazi wa eneo hilo kuwa macho huku wakifunga eneo hilo kudhibiti majanga yoyote.