Habari Mseto

Wasiwasi wa chifu huenda idadi kubwa ya waliofaa kukamilisha elimu mwaka huu wakakosa kurejea shuleni 2021

August 24th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

HUENDA idadi kubwa ya wanafunzi ambao wangekamilisha elimu yao ya kiwango cha kidato cha nne na darasa la nane mwaka huu wa 2020 ulioathiriwa na janga la Covid-19, wakashindwa kuendelea na masomo mwaka 2021, amesema afisa mmoja.

Kulingana na chifu wa Tiwi katika Kaunti ya Kwale Bw Nassor Kuphuma, watoto wengi wanajihusisha na ajira.

Bw Kuphuma alisema wengi wa wanafunzi kwa sasa wanajihusisha na ajira za mapema ili kujikimu kimaisha.

Kazi hizo alisema ni kama vile  uchukuzi wa bodaboda na wengine wakifanya kazi za nyumbani.

Chifu huyo alitoa wito kwa wazazi walio na wanafunzi hao kuhakikisha wanawapa hamasa ili kuona kuwa wanazingatia masomo japo shule zingali zimefungwa kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

“Tunaomba wazazi musisitizie wanafunzi umuhimu wa kudurusu. Kuna baadhi kufuatia utamu wa pesa watakosa kurudi shuleni kukamilisha masomo katika viwango vyao mbalimbali,” akasema.

Aidha aliwahimiza wakazi wakome kuajiri watu walio chini ya umri wa ajira; yaani ule ambao si wa utu ukubwani.

Alisema yeyote ayakayepatikana akiajiri watoto atachukuliwa hatua kisheria.

Aidha aliwaonya wanaowapa watoto wasio na leseni kazi, akisema kufanya hivyo kutachangia kuongezeka kwa ajali za barabarani.