Kimataifa

Wasiwasi wa sekta ya binafsi kuhusu fursa za biashara barani Afrika

November 26th, 2019 2 min read

Na KEN WALIBORA akiwa ADDIS ABABA, Ethiopia

UKOSEFU wa habari huenda ukawa ndiyo changamoto kubwa zaidi inayotatiza kuhusika kwa sekta ya binafsi katika Muafaka wa Soko Huria Barani Afrika, (AfCFTA).

Hata hivyo, itakuwa vigumu kwa serikali za Kiafrika kupata matunda ya soko huria hili na kujikwamua kutoka kwa minyororo ya ushawishi wa mabara mengine, bila mchango wa sekta ya binafsi.

Wakizungumza katika kikao kilichoandaliwa na Muungano wa Afrika, (AU), na Umoja wa Mazungumzo kuhusu Afrika (CoDA), jijini, Addis Ababa, Ethiopia, wadau wa sekta ya binafsi, wakiwemo maafisa wa vyama vya wenye biashara na viwanda, walilalamikia kupuuzwa na serikali zao katika maamuzi muhimu barani Afrika.

Wajumbe hao walikuwa na maswali mengi yaliyoashiria wasiwasi wao kuhusu utekelezaji wa vipengele vya Mwafaka huo wa Soko Huria Barani Afrika.

Walitaka kujua na walijibiwa ipasavyo, ni bidhaa gani itakayouzwa, jinsi ukakavyokuwa mfumo wa ulipaji baina ya nchi za Kiafrika, na vile nchi hizo zitavyotekeleza mwafaka huo kabla Julai 2020, wakati ambapo mwafaka huo utaanza kutekelezwa ipasavvyo.

Aidha wajumbe walielezea wasiwasi wao kuhusu utayari wa serikali zao kushirikiana na sekta ya binafsi na vyuo vikuu katika utafiti utakaofanikisha utekelezaji wa Mwafaka huo wa Soko Huria Barani Afrika.

 

Mshauri wa Kiufundi wa Chama cha Wenye Biashara na Viwanda Kenya kwenye kikao cha AfcFTA jijini Addis Ababa, Ethiopia. Picha/ Hisani

Wajumbe kwenye kikao hicho walihofia kwamba watu wasiokuwa Waafrika wanaweza kujipenyeza moja kwa moja au kiujanja kwa kupitia washirika wa Kiafrika katika biashara kati ya mataifa ya Afrika inayopaswa kuwa ya Waafrika pekee kwa ajili ya Waafrika.

Wawakilishi wa sekta ya binafsi walisema kwamba sekta hiyo ndiyo mhimili mkubwa wa kubuniwa kwa nafasi za ajira kutokana na uwekezaji. Kwa hiyo, ipo haja kwa serikali kuwaihusisha zaidi sekta hii na wadau wake, badala ya kuwapuuza mbali na kuweka vizuizi visivyokuwa na msingi kama kuzuia upatikanaji wa baadhi ya taarifa muhimu.

Kamishna wa Muungano wa Afrika anayehusika na Biashara na Viwanda, Albert Muchanga, alitoa wito wa kuwapo uwazi na ujitoleaji miongoni mwa wadau.

Kamishna Muchanga alisisitiza umuhimu wa kushirikishwa kwa sekta binafsi katika utekelezaji wa mwafaka huo kwa vile sekta hiyo ndio uti wa mgongo wa biashara ya ndani ya bara hili.

Aliwataka wadau wa sekta binafsi kubadili mwelekeo kuhusu fursa za biashara barani Afrika mbali na kubainisha bila hofu visa vya ufisadi vinavyolemaza maendeleo ya kiuchumi.

Mshauri wa Kiufundi wa Chama cha Wenye Biashara na Viwanda nchini Kenya, Peter Kamau, aliwahimiza wadau wa sekta ya binafsi kuziendea serikali zao na ushauri wao wakishapuuzwa badala ya kujikunyata tu.

Kwenye kikao hicho cha Jumatatu alasiri, Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mazungumzo kuhusu Afrika, (CoDA), kilichoandiliwa na Souad Aden-Osman, majadiliano ya awali kuhusu kuundwa kwa majopo-kazi ya AfCFTA yalifanyika huku kikao kingine cha aina hiyo kikiratibiwa kufanyika Accra, Ghana mnamo Januari mwakani.

Mwafaka wa Soko Huria Barani Afrika ulipasishwa rasmi mnamo Mei 30, 2019 na utaanza kutekelezwa mnao Julai 2020.