Habari za Kaunti

Wasiwasi wakulima wa nafaka Bondeni wakifikiwa na KRA

February 20th, 2024 2 min read

NA BARNABAS BII

TAHARUKI imegubika wakulima wa nafaka katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa kuhusiana na mpango maalum wa kukusanya ushuru uliozinduliwa na Mamlaka ya Kukusanya Ushuru Nchini (KRA).

Mfumo huo wa Kudhibiti Malipo ya Ushuru Kielektroniki (eTims), utahitaji wakulima kutoa rekodi zao za hesabu kuhusu fedha wanazotumia kununua vifaa vya kilimo na mauzo.

Idadi kubwa ya wakulima walisema jana kuwa hawana ujuzi wa kutumia intaneti ili kuwawezesha kuhifadhi rekodi za hesabu kuhusu kiasi wanachowekeza katika uzalishaji na mapato kutokana na mimea.

“Mfumo huo unawafaa wakulima wa mijini na waliosoma wenye uwezo wa kupata intaneti, simu za kisasa na kuweka rekodi za hesabu lakini unaweza kuwaathiri wakulima wa vijijini ambao hawana simu wala intaneti,” walisema wakulima hao wakiongozwa na Bw Kipkorir Menjo katika mkutano uliofanyika mjini Eldoret.

Hazina Kuu imepanga kuanzisha ushuru wa asilimia tano utakaotozwa mazao ya shamba yanayouzwa kwa vyama vya ushirika na viwanda vya bidhaa za kilimo, katika juhudi za kuongeza ushuru unaokusanywa.

Katika mfumo mpya, biashara zinahitajika kutoa nakala ya kielektroniki kuhusu shughuli zote wanazotekeleza la sivyo haziwezi kuitisha fedha walizotumia wakati wa kujaza Ushuru wa Mapato.

KRA imezindua mipango ya uhamasishaji inayolenga wakulima na wafanyabiashara kuhusu mfumo mpya unaotarajiwa kuanza mwezi ujao.

“Baadhi ya wakulima hawajajiandikisha na vyama vya ushirika na wanahitaji uhamasishaji mwingi kabla ya mfumo mpya wa ushuru kutekelezwa,” alisema Bw Jackson Kemboi kutoka Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.

Baadhi ya wenye viwanda katika eneo la Magharibi, sasa wanahofia kukatwa ushuru kuhusiana na fedha walizolipa wakulima kwa matumizi yaliyofanyika bila eTims.

Kulingana na wenye viwanda, KRA haijafafanua kuhusu matumizi ya fedha yaliyotekelezwa kabla ya Machi 31, 2024, ambapo biashara zote zitatekelezwa kupitia rekodi za kielektroniki, eTims, baada ya Mswada wa Fedha 2023, kupitishwa kuwa sheria.

“Itakuwaje kuhusu mazao yaliyonunuliwa kutoka kwa wakulima bila eTims kati ya Januari 1 na Machi 31? Je, wamiliki viwanda watahitajika kugharamia ada hizo hivyo kuwasababishia hasara kuu? Aliuliza Mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki Viwanda, KBw en Nyaga.

Amerai KRA kuwaondolea wenye viwanda ada zinazohusu shughuli zozote walizotekeleza kabla ya mwezi ujao.