Habari Mseto

Wasiwasi wakumba familia baada ya mzee kupotea

October 2nd, 2019 1 min read

Na SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA

FAMILIA moja katika kijiji cha Ikonyero, kata ya Kambiri, tarafa ya Lubao, Kaunti ya Kakamega inaishi kwa hofu na wasiwasi baada ya baba yao mwenye umri wa miaka 75 kutoweka Agosti 2019 na mpaka sasa haijabainika aliko.

Mzee huyo ambaye ni kiziwi aliripotiwa kutoweka nyumbani kwake mnamo Agosti 15 na licha ya kusakwa na wanakijiji pamoja na maafisa wa polisi, hajapatikana.

Bw Eliakim Zakiel Amukongo aliondoka nyumbani kwenda kuhudhuria mazishi ya kakake Peter Jumba katika wadi ya Chekalini, kaunti ndogo ya Lugari lakini hajarejea nyumbani mpaka sasa.

Ilisemekana kuwa baada ya mazishi alianza mwendo kurejea nyumbani lakini miezi miwili baadaye hajaonekana.

Mzee huyo mwenye urefu wa futi sita mwisho alionekana amevalia koti la kahawia (brown), shati jeupe na tai yenye rangi ya samawati.

Mwanawe wa kiume, Wycliffe Amukongo anasema baba huyo wa watoto watano huwasiliana kwa kutumia lugha ya ishara kwa sababu ni kiziwi na hana uwezo wa kuongea.

“Tulidhani alikuwa ameenda kwa majirani, marafiki au jamaa zetu. Tumeuliza watu wetu wote lakini hawajamwona. Tumejawa na hofu kwamba huenda alipotea pahala fulani,” akasema.