Habari

Wasiwasi wazuka baada ya makundi ya Mungiki, Gaza kuungana

October 28th, 2019 2 min read

Na TAIFA RIPOTA

TAHARUKI imezuka upya katika eneo la Kati kufuatia habari za kuungana kwa makundi ya uhalifu ya Gaza na Mungiki.

Kulingana na duru za usalama, vijana wanaoaminika kuwa wa kundi la Gaza sasa wako chini ya mmoja wa waliokuwa viongozi wakuu wa Mungiki.

Vijana wa kundi la Gaza, ambalo chimbuko lake ni mtaa wa Kayole jijini Nairobi, wanaripotiwa kupanua shughuli zao hadi mitaa mingine ya Nairobi, Kiambu, Nyeri na Murang’a ambapo wanaendesha shughuli za kukusanya ada haramu kutoka kwa wahudumu wa matatu na kutuma sehemu ya pesa hizo kwa mmoja wa waliokuwa waanzilishi wa Mungiki.

Naibu Kamishna wa Juja, Charles Mureithi aliambia mkutano wa usalama eneo hilo kuwa vijana hao kutoka Kayole, Murang’a, Githurai na Kahawa West pia wanaendesha shughuli ya kusajili wafuasi zaidi wakiwemo wasichana katika miji ya Juja na Githurai Kimbo.

“Tunafuatilia kwa makini shughuli za vijana hawa. Tunajua mienendo yao na hatutawavumilia. Tuna habari kuwa wanakusanya pesa na kuzituma kwa mmoja wa viongozi wa Mungiki,” akasema Bw Mureithi.

Kwa muda sasa kumekuwa na ripoti za kuchipuka upya kwa kundi la Mungiki lakini kuungana kwake na Gaza kumeonekana kuchukua mkondo hatari ikizingatiwa ukatili wa makundi hayo mawili dhidi ya wananchi wa kawaida.

Katika kaunti za Murang’a na Kiambu, wafuasi wa Mungiki wameanzisha upya tabia zilizokuwa zikitekelezwa na kundi hilo kabla ya kukabiliwa vikali na aliyekuwa Waziri wa Usalama wakati huo marehemu John Michuki.

Wasimamia huduma za matatu

Wafuasi hao wameanza kusimamia huduma za matatu ambapo wanakusanya ada za kila siku na pia kuamua wanaofaa kuhudumu maeneo fulani.

Kamishna wa Kaunti ya Murang’a, Mohammed Barre wiki iliyopita alikiri kuwa wafuasi wa Mungiki wamechukua udhibiti wa shughuli za matatu zinazohudumu maeneo ya Kaharati, Muthithi, Kigumo na Kangari.

Kundi hilo limeripotiwa kudai Sh4,000 kutoka kwa makanga, dereva Sh6,000 na mwenye matatu Sh40,000 kabla ya kuruhusiwa kubeba abiria eneo hilo.

Wakazi waliambia Taifa Leo kuwa watu kadha ambao wamekaidi masharti ya kundi hilo wameuawa ama kulazimika kuhama eneo hilo.