Habari Mseto

Wasomaji wa Kiswahili wapenzi wa Taifa Leo wakongamana mjini Voi

November 9th, 2019 2 min read

Na LUCY MKANYIKA

WANACHAMA wa Chama cha Wasomaji wa Kiswahili wa Taifa Leo (WAKITA) wanakongamana kwenye kikao cha Jumamosi mjini Voi.

Mkutano huo wa Jumamosi umejadili mbinu za kuvumisha Kiswahili kote nchini.

Wakiongea mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta, wakati wa kongamano lao la mwisho wa mwaka, viongozi wa chama hicho wamesema kuwa watatembelea kaunti zote 47 ili kukutana na wasomaji wa gazeti hilo.

Zaidi ya wasomaji na wapenzi wa Kiswahili 200 wamehudhuria kikao hicho ambacho waandishi wa Taifa Leo na viongozi wa WAKITA wamehudhuria.

Mwenyekiti wa chama hicho nchini Dkt Abdul Nur amesema kuwa chama hicho kimeweza kuboresha lugha ya Kiswahili nchini kupitia gazeti hilo.

“Lengo letu ni kuboresha lugha hii; hasa shuleni, vyuoni na miongoni mwa wananchi kwa ujumla,” amesema Dkt Nur.

Aidha ameeleza kwamba lugha hiyo huunganisha Wakenya na hivyo inaweza kutumika kuondoa kadhia ya ukabila unaoendelea kuleta mgawanyiko miongoni mwa Wakenya.

Mshirikishi wa chama hicho katika eneo la Pwani Bw Kinyua Bin King’ori amesema kuwa lugha hiyo imeboresha utumizi wa lugha ya Kiswahili nchini na hivyo kuinua maisha ya Wakenya.

“Maisha ya watu wengi yameimarika kutokana na lugha hii. Ninawahimiza Wakenya kupenda Kiswahili kwani ndiyo lugha rasmi ya nchi yetu,” amesema Bw Bw Kinyua.

Ushirikiano

Mhariri wa Taifa Leo Bw Peter Ngare amesema kuwa watashirikiana na chama hicho ili kuboresha gazeti hilo.

Amesema kuwa gazeti hilo litajitahidi kunasa vipaji mbalimbali vikiwemo watunzi wa mashairi, waimbaji wa nyimbo na sanaa mbalimbali za wanachama wa Wakita.

“Nyinyi ni viungo muhimu sana kwa gazeti hili ndiposa tumehudhuria kikao hiki ili kujumuika nanyi,” amesema Bw Ngare.

Amekitaka chama hicho kushirikisha gazeti hilo katika mipango yao kadha wa kadha kwa lengo la kuboresha makala mbalimbali na jinsi habari zinavyoandikwa katika gazeti hilo na majarida yake.

Aidha, Bw Ngare amesema kuwa hivi punde gazeti hilo litaanza kuchapisha jarida mahususi la Pwani sawia na la bara ili kuwapa wasomaji habari za maeneo yao na yanayoendana au kulandana na maisha yao ya kila siku.

Vilevile, ameahidi kuwa baadhi ya kurasa ambazo ziliondolewa baada ya gazeti hilo kufanyiwa mabadiliko zitashughulikiwa.

Mwakilishi wa wadi ya Kaloleni Bw Omar Ahmed amesema kuwa atashirikiana na chama hicho kuboresha lugha ya Kiswahili hasa kupitia gazeti la Taifa Leo.

“Lugha hii ni muhimu sana katika kuboresha maisha ya wananchi. Tunatambua hili na tuko tayari kushirikiana nanyi,” amesema diwani Ahmed.