Wasomali 4 wanaswa UG

Wasomali 4 wanaswa UG

Na DAILY MONITOR

POLISI nchini Uganda wanazuilia raia wanne wa Somalia, kwa madai ya kupanga njama ya kulipua mkutano wa Rais Yoweri Museveni hotelini.

Msemaji wa Polisi Fred Enanga jana alisema kuwa, washukiwa walipatikana na kifaa cha kulipulia bomu ndani ya gari, karibu na hoteli ya Speke Munyonyo.Kifaa hicho kiligunduliwa wakati maafisa wa usalama wakikagua gari hilo.

Tukio hilo linajiri wiki moja baada ya magaidi kutekeleza mashambulio mawili kwa mpigo, karibu na kituo cha polisi cha Central na majengo ya Bunge jijini Kampala. Watu wanne, wakiwemo polisi wawili, waliuawa.Kundi la kigaidi la Islamic State (IS) lilidai kuhusika na shambulio hilo, lililotekelezwa na watu wa kutoa mhanga walioabiri pikipiki.

Serikali ya Uganda ilisisitiza kuwa milipuko hiyo ilitekelezwa na kundi la Allied Democratic Forces (ADF), ambalo ni mshirika wa IS.Kundi la ADF linaendesha shughuli zake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“Maafisa wa kupambana na ugaidi wamenasa raia wanne wa Somalia. Walipata kifaa cha kulipua bomu. Sasa tumeanza operesheni ya kutafuta bomu lenyewe,” alieleza Enanga.Rais Museveni anatarajiwa kukutana na mawaziri pamoja na wakuu wa serikali katika hoteli hiyo ya Speke Munyonyo.

Amekuwa akifanya mikutano katika hoteli hiyo kwa miaka mingi.Wiki iliyopita, watu watano – akiwemo mhubiri wa Kiislamu, Sheikh Muhammad Abas Kirevu – waliuawa kwa risasi na wengine zaidi ya 20 kukamatwa katika operesheni kali dhidi ya ugaidi.Rais Museveni pia aliagiza kusakwa kwa mhubiri mwingine wa Kiislamu, Sheikh Suleiman Nsubuga.

Wasomali hao walinaswa siku moja baada ya Enanga kusema kuwa, watoto 80 wameokolewa kutoka vituo vya usajili wa mafunzo ya kigaidi, tangu wiki jana.Kulingana na Enanga, maafisa kutoka kwa jopo la kupambana na ugaidi na wale wa Idara ya Ujasusi (CMI) jeshini walivamia vituo vinavyodai kuendesha usajili huo katika maeneo ya Kalule, Luwero na Ntoroko ambako watoto 50 waliokolewa.

Jumatano na Alhamisi wiki jana, washukiwa watano wanaoendesha mafunzo walikamatwa.Mwishoni mwa wiki jana, uvamizi mwingine uliendeshwa katika eneo la Kasengeje, katika Wakiso.Hii ni baada ya maafisa wa usalama kupata habari kwamba mkuu wa kituo hicho Sheikh Rwangabo alikuwa akileta watoto kutoka maeneo mbalimbali jijini Kampala na Wilaya ya Wakiso.

Rais Museveni kwa sasa anafanya mazungumzo na mwenzake wa DRC, Rais Felix Tshiekedi juu ya uwezekano wa kupeleka wanajeshi wa Uganda mashariki mwa DRC kupambana na kundi la ADF.Ripoti ya Ofisi ya Pamoja ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilionyesha kuwa kati ya Januari 2019 na Juni 2020,watu 1,066 waliuawa na watoto 59 waliosajiliwa katika kundi la ADF kwenye majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri.

ADF ilibadilika na kuwa kundi lenye mtazamo wa kimataifa zaidi baada ya Musa Baluku, raia wa Uganda mwenye umri wa kati ya miaka 40, kurithi uongozi wa ADF baada ya kukamatwa na kurejeshwa nchini Uganda mwanzilishi wake Jamil Mukulu.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Matamshi ya Ruto kwa hakika...

TAHARIRI: Polisi waangalie upya mishahara ya maafisa wao

T L