Wasomi 29 hatarini kuuawa na majambazi waliowateka nyara

Na MOHAMMED MOMOH

Mwandishi wa Nation, Afrika Magharibi

LAGOS, NIGERIA

WAFUASI wa genge moja la wahalifu wametisha kuwaua wanafunzi 29 waliowateka nyara baada ya serikali ya Nigeria kukataa kulipa ridhaa ya Naira 300 milioni (Sh1.2 bilioni) ili wawaachilie huru wanafunzi hao.

Wanafunzi hao wa chuo cha Federal College of Forestry Mechanisation, kilichoko katika jimbo la Kaduna walitekwa nyara Machi 11, 2021. Wahuni hao walitaka ridhaa hiyo ilipwe na serikali ya jimbo la Kaduna.

Wanafunzi 10 waliachiliwa huru baada ya wazazi wao kulipa ridhaa. Lakini 29 waliosalia wangali wanazuiliwa kwa sababu Gavana Nasir El-rufai wa jimbo la Kaduna amekataa kushauriana na watekaji nyara hao licha ya wazazi wao kuomba mara kadha kwamba serikali izungumze na majambazi hao.

Mwakilishi wa wazazi hao, Bw Friday Sanni mnamo Aprili 16, 2021, alisema wamekuwa wakipata simu kutoka kwa watekaji nyara hao wakitisha kuwaua wanafunzi wa kiume na kuwaoa wale wa kike.

“Tunatoa wito kwa Serikali ya Nigeria, mashirika yasiyo ya kiserikali na wafadhili watusaidie kutoa fedha za kuokoa watoto wetu,” akasema Sanni.

“Wahalifu hao wametisha kuwaua watoto wetu. Serikali nayo inasema kuwa mzazi yeyote atakayefanya mazungumzo na majangili watashtakiwa,” akaongeza.

Serikali ya jimbo la Kaduna imeonya kwamba, haitakubali vitisho kutoka kwa wahalifu hao kuhusu hatima ya wanafunzi hao.

Kamishna wa Usalama wa Ndani na Masuala ya Nyumbani, Bw Samuel Aruwan, mnamo Aprili 6, 2021 akasema hivi: “Serikali itaongeza juhudi za kuhakikisha visa vya ujangili na utekaji nyara vimezimwa bila kukubali ‘vitisho na kuingizwa siasa kwa tukio hilo la kusikitisha’”

Alikanusha madai kuwa Gavana Nasir El-Rufau alitisha kuwafungulia mashtaka mzazi yeyote ambayo ataamua kufanya mazungumzo na walihalifu hao ambao wamewaweka mateka watoto wao.

“Gavana hatafanya mazungumzo na hatalipa ridhaa kwa majangili hao,” akakariri.

Alieleza kuwa “kuna watu ambao wamekuwa wakidai kuwa wameteuliwa na serikali kufanya mazungunzo na wahalifu hao kwa niaba yake.”

“Hawa ni waongo na ni matapeli wakubwa,” akasema Bw Aruwan.

Wakati huo huo, nyingi za shule 1,029 zilizofungwa ili kuzuia visa vya kutekwa nyara kwa wanafunzi katika majimbo ya Sokoto, Zamfara, Kano, Katsina, Niger na Yobe kaskazini mwa Nigeria zimefunguliwa.