Wasomi waanza kupigania uvaaji wa hijab shuleni

Wasomi waanza kupigania uvaaji wa hijab shuleni

NA DERICK LUVEGA

WATAALAMU wa kike wa Kiislamu wanawazia kubuni sheria itakayowezesha wanafunzi kuvaa hijab shuleni.

Hii ni baada ya usimamizi wa taasisi za elimu kukosa kutekeleza amri iliyotolewa na Wizara ya Elimu inayoruhusu matumizi ya vazi hilo la kidini kwa wanafunzi wa Kiislamu katika shule za msingi na za upili.

Wakiongozwa na kamishna wa Tume ya Mgao wa Mapato (CRA) Hadija Nganyi, wataalam hao walisema watapigia debe ajenda hiyo kupitia kundi lao la Wataalamu Wanawake Waislamu.

Walisema haya katika Shule ya Sekondari ya Bo Yusuf Muslim, Kaunti ya Vihiga wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya Sikukuu ya Hijab Duniani.

Bi Nganyi alisema kundi hilo linaungwa mkono na Mbunge Maalum, Bi Zamzam Muhammed na Waziri wa Ulinzi, Aden Duale.

Walisema Bi Muhammed atasaidia kushinikiza kubuniwa kwa sheria hiyo kupitia Bunge la Kitaifa kwa kupendekeza mswada huo huku Bw Duale akisaidia kupitia utawala.

Haya yamejiri zaidi ya mwezi mmoja baada ya Bw Duale kuvutia hisia mseto alipowaonya wanawake Waislamu Wakenya wasiovaa vazi hilo la kufunika kichwa kutafuta nchi nyingine ya kuishi.

Bi Nganyi alisema kundi hilo pia litawasiliana na Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu ili kushinikiza utekelezaji wa sheria kuhusu hijab.

Sheria hiyo iliwekwa mwaka 2022 lakini wanawake Waislamu wana wasiwasi kuwa walimu wakuu wa shule watawafukuza wasichana wanaotumia vazi hilo.

Jambo hili, wanasema, linawafungia nje ya shule wasichana wengi Waislamu hivyo basi kuwanyima haki ya kupata elimu.

“Ni muhimu tuzungumze ili kuhakikisha kuwa mambo yanafanyika ipasavyo. Tumepokea malalamishi kwamba watoto Waislamu hawaruhusiwi kuvalia hijab,” alisema.

“Wizara ya Elimu imeruhusu uvaaji wa hijab lakini usimamizi wa shule umekaidi,” alisema.

“Pana haja ya kuhamasisha shule ili elimu ya wasichana isiathirike. Hata polisi na jeshi hawaruhusiwi kulivalia.”

Zaidi ya wasichana 100 katika Shule ya Sekondari ya Bo Yusuf walikabidhiwa hijab wakati wa sherehe hizo.

Bi Nganyi alisema wanataka serikali itekeleze sheria kuhusu uvaaji wa mavazi ya kidini.

Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kaimosi Friends (Kafu), Bi Fauzia Noorwin, alisema wakati umewadia wa kupigania haki za Waislamu ili kuwezesha mtoto wa kike kupata elimu.

Alisema kundi hilo la waliotengwa linateseka huku wasichana wachache wa dini hiyo wakipata elimu.

Alisema kwa mfano, Kaunti ya Vihiga ina Waislamu wwanawake wasiofika 50 ambao wana digrii ya uzamili.

Aidha, alisema eneo zima la Magharibi mwa Kenya lina wanawake wasiofika watano walio na shahada ya uzamifu.

“Ni sharti Waislamu wapiganie haki zao. Wazazi na wanafunzi wanaokabiliwa na pingamizi kuhusi uvaaji wa hijab wanapaswa kuripoti. Tunataka watu wetu kuwepo kwenye bodi za shule ili haki hii ipigiwe debe na kutekelezwa,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Spika Wetang’ula awataka wabunge wapitishe sheria ya...

Ushonaji mikeka waokoa wanawake kiuchumi Lamu

T L