Habari Mseto

Wasomi wadai mtaala mpya wa elimu utazidisha ukabila

April 12th, 2018 1 min read

Msomi wa Lamu, Abdalla Fadhil. Asema mtaala mpya wa elimu hapa nchini huenda ukawa ndoto kutekelezwa kutokana na kwamba umekopi mambo mengi ya mataifa ya magharibi. Pia anahoji kwamba kufundishwa kwa lugha ya mama shuleni kutachangia ukabila na mgawanyiko zaidi hapa nchini. Picha/ Kalume Kazungu

NA KALUME KAZUNGU

WASOMI wa Lamu wamelalamikia mtaala mpya wa elimu uliozinduliwa mwaka huu hapa nchini wakidai huenda mfumo huo ukachangia pakubwa kuzidisha ukabila nchini.

Wasomi hao kadhalika wanadai mtaala huo uliundwa kwa kuiga tamaduni za mataifa ya magharibi, hivyo  huenda ikawa vigumu kwa mtaala huo kutekelezwa ipasavyo hasa kwenye shule nyingi za umma hapa nchini.

Wakiongozwa na Bw Abdalla Fadhil, wasomi hao walitaja kufundishwa kwa lugha ya mama shuleni kuwa miongoni mwa vigezo vikuu vitakavyochangia mgawanyiko zaidi hapa nchini.

Walisema ipo haja ya Wizara ya Elimu kufanya mageuzi ya kina kuhusiana na mtaala huo, wakihoji kwamba huenda ikawa ndoto kutekelezwa kwa mfumo huo wa elimu.

“Ninavyofahamu ni kwamba mtaala huo mpya umekopi mambo mengi kutoka nchi za magharibi. Kuna vitu vingi ambavyo vimepachikwa tu bila kuzingatia miundomsingi kwenye shule zetu.

Kwa mfano, ni shule ngapi ziko na uwanja au vifaa vya kuendelezea michezo ya tenisi na masuala mengine? Pengine shule za kibinafsi pekee.

Pia ninasikitika kwamba lugha ya mama imepitishwa kama somo litakalofundishwa kwenye shule zetu. Hilo ni jambo litakalochangia ukabila na mgawanyiko zaidi hapa nchini. Mtaala wetu uangaziwe la sivyo itakuwa ndoto kuutekeleza,” akasema Bw Fadhil.

Naye Bw Yusuf Abdulkadir alieleza hofu kwamba mtaala huo utapelekea kufifia kwa tamaduni za hapa nchini, ikizingatiwa kuwa mambo mengi yanayojumuishwa na kupewa kipaumbele ni yale ya mataifa ya magharibi.

Pia alisema kujumuishwa kwa somo la lugha ya mama ni ndoto kwa eneo kama vile Lamu, ambako lugha zinazoongewa zinakanganya.

“Wanasema wataka kufunza lugha ya mama shuleni. Mahali kama vile Lamu watafundisha lugha gani? Hapa kuna Kiswahili cha Kibajuni.

Kibajuni chenyewe kimegawanyika. Kuna kile cha Pate, Ndau, Kizingitini, Siyu na sehemu zingine. Watafundisha lugha gani ya mama maeneo kama hayo? Ninahisi mtaala huo ni ndoto tu za Abunuasi,” akasema Bw Abdulkadir.