Makala

WASONGA: Bajeti inayosomwa leo haijali athari za corona

June 11th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

BAJETI ya kitaifa inaposomwa leo bungeni kuna maswali mengi ibuka kuhusiana na viwango vya fedha zilizotengewa mipango muhimu na sekta kuu, ambazo zinatarajiwa kupiga jeki uchumi wakati huu wa janga la Covid-19.

Inasikitisha kuwa ingawa Mei Waziri wa Fedha Ukur Yatani aliweka wazi kwamba kwa wastani, uchumi wa Kenya utakuwa ukipoteza Sh60 bilioni kila mwezi kutokana na janga hili, mipango wa kukabiliana na makali yake imetengewa Sh53.7 bilioni pekee.

Hii ni licha ya kwamba bajeti itakayosomwa leo ni ya Sh2.73 trilioni ambapo fedha nyingi zimetengewa miradi na sekta ambazo, kwa hakika, hazina dharura na umuhimu mkubwa nyakati hizi.

Sh53.7 bilioni ni pesa zile zile ambazo Rais Uhuru Kenyatta alitangaza Mei alipoweka wazi mpango wa kuchochea uchumi ili kupunguza makali ya janga la corona.

Inaonekana kwamba maafisa katika Hazina ya Kitaifa na wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti walipuuza kabisa ushauri wa wataalamu kwamba mpango wa kupambana na janga hili ulipasa kutengewa takriban Sh200 bilioni ili uweze kufaidi watu wengi.

PESA ZISIZOFAA

Mataifa mengi barani Afrika na mabara mengine, yametenga kiwango kikubwa zaidi cha fedha kwa mpango wa kukabiliana athari za Covid-19; mfano ikiwa Rwanda ambayo limetenga Sh280 bilioni kwa mpango huo.

Inakera hata zaidi kwamba licha kwamba Wizara ya Afya ndiyo iko mstari wa mbele katika vita dhidi janga la corona, imetengewa Sh111.7 bilioni pekee. Hii ni baada ya wabunge wanachama kamati ya bajeti kupunguza Sh3 bilioni kutoka mgao wa awali wa Sh114.7 bilioni.

Ukweli ni kwamba, wakati huu ambapo maambukizi ya virusi vya corona yanashuhudiwa katika ngazi za jamii, wizara hii inayoongozwa na Bw Mutahi Kagwe inahitaji bajeti kubwa zaidi ili iweze kukabiliana na hali hiyo.

Inahitaji fedha za kununua vifaa vya kupima corona katika maeneo ya mashinani, ikizingatiwa kuwa serikali za kaunti zimeonekana kulemewa na mzigo huo.

Pia kuna mpango wa kuajiri na kutoa mafunzo maalum kwa wahudumu wa afya wa kijamii (CHW) ili waweze kuendeleza mpango wa upimaji na utengaji wa watu waliopatikana na virusi vya corona.

Kimsingi, hakuna mantiki yoyote ya Wizara kama ya Ulinzi kutengewa Sh115 bilioni ilhali taifa hili halikabiliwa na tishio lolote la kushambuliwa na mataifa ya kigeni. Vile vile, haieleweki ni kwa nini kando na mgao huo, Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) limetengewa Sh39 bilioni ilhali Wizara ya Usalama wa Ndani tayari imetengewa Sh131 bilioni.

Vile vile, mbona Afisi ya Rais imetengewa kiasi kikubwa cha Sh36.6 bilioni ilhali wakati huu ambapo Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto hawafanyi ziara nyingi za humu nchini na kimataifa kama ilivyokuwa zamani Kwa mfano siku hizi Rais Kenyatta huendesha mikutano ya kimataifa kupitia mitandao ya Zoom au Skype.

Na sio jambo la busara kwa serikali kutenga jumla ya Sh904.7 bilioni kwa ajili ya kulipa madeni ya humu nchini na kimataifa badala ya serikali kujadiliana na wadeni wake ili kuahirisha ulipaji wa baadhi ya madeni.