MakalaSiasa

WASONGA: Dkt Ruto atii agizo la Rais na kusitisha ziara za kisiasa

April 28th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MWAKA 2018 Rais Uhuru Kenyatta alipiga marufu uzinduzi wa miradi mipya ya maendeleo yanayofadhiliwa na serikali kuu ili kutoa nafasi kukamilishwa kwa miradi ilianzishwa zamani lakini haijakamilishwa.

Pili, aliwataka wanasiasa na maafisa wakuu serikalini kukoma kufanya ziara zisizo na maana maeneo mbalimbali nchini wakichapa siasa kwa kizingizio cha kukagua miradi ya maendeleo.

Lakini inaonekana kuwa Naibu Rais William Ruto amekaidi amri hii kwani amekuwa akizunguka kote nchini akiandama na wabunge kadhaa kwa kisingizio cha kukagua miradi ya maendeleo na kuzindua mingine mipya.

Inaonekana kuwa Rais Kenyatta ameng’amua hili ndiposa akaonya maafisa wa usalama na utawala dhidi ya kuhudhuria baadhi ya mikutano hiyo.

Isitoshe, baadhi ya wabunge wandani wake wameanza kutishiwa kwa kupokonywa walinzi kuashiria kuwa mienendo yao inaenda kinyume na misimamo ya Rais na serikali yake.

Huu mtindo wa uzinduzi wa miradi ya maendeleo kiholela una madhara makubwa kwa uchumi wa nchini na Dkt Ruto na wenzake wanapaswa kung’amua ukweli huu.

Hii ni kwa sababu mapapa hawa wamekuwa wakitumia miradi hii kama njia ya kupora pochi la taifa na kutumia pesa hizi kununulia wapigakura.? Ama kwa hakika kati ya laana zinazotafuna uchumi wetu ni ule utamanduni wa kutumia miradi ya serikali kama nyenzo ya kupora mali ya umma.

Ni utamaduni unaotumiwa na wanasiasa na maafisa wakuu serikalini kujitafutia mabilioni ya pesa za kufadhili siasa zao. Wanasiasa hawa vigogo hushirikiana na wafadhili wa kigeni wenye nia ya kupunguza umaskini kwao na kuongeza umaskini kwetu.

Wafadhili hawa wa kigeni ikiwa ni pamoja na serikali, wanatumia ‘ujinga’ wa viongozi wa Afrika kujipatia faida za kushangaza. Kwa upande mwingine wanatia mataifa husika katika mtego wa madeni na utegemezi.

Hili ndilo Rais Kenyatta amedhamiria kwa kupiga marufuku kampeni za urais 2022 kwani zinayumbisha nchi yetu.

Bila shaka kampeni hizi huendeshwa kwa mabilioni ya pesa zilizotengewa miradi au ushuru wa wananchi.? Miradi hii husaidia wanasiasa hawa kuua ndege wawili kwa jiwe moja.

Pili, na muhimu zaidi, ni njia ya kijanja ya kuwawezesha wao na washirika wao, kupora mabilioni ya pesa kwa jina la kuletea wananchi maendeleo.

Bila shaka Rais Kenyatta anaelewa kuwa mzigo wa sasa wa deni ni jumla ya Sh 5.4 trilioni sio himilivu tena.

Na hii ndio maana China imedinda kutuongezea deni lingine la kujenga reli ya kisasa (SGR) kutoka Naivasha hadi Kisumu.