WASONGA: EACC itaje wazi watumishi wa umma wachapao siasa

WASONGA: EACC itaje wazi watumishi wa umma wachapao siasa

Na CHARLES WASONGA

KILA Mkenya ana haki ya kuwania kiti chochote cha kisiasa katika uchaguzi mkuu mradi ametimiza mahitaji yanayohitajika kisheria.

Lakini kuna sheria na kanuni, zinazoongoza taratibu za uchaguzi haswa endapo wale ambao wangetaka kushiriki katika shughuli hizi ni watumishi wa umma.

Kulingana na Sheria za Uchaguzi zinazotumika sasa, watumishi wa umma wanahitajika kujiuzulu miezi sita kabla ya tarehe ya uchaguzi mkuu.

Hii ndio maana katika mwongozo uliotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) watumishi wa umma ambao wanataka kuwania viti sita vitakavyoshindaniwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 9, 2022, watahitajika kujiuzulu ifikapo Februari, mwaka ujao.

Kabla ya hapo, watumishi wa umma wenye ndoto za kisiasa hawafai kuanza kampeni za mapema za kujitafutia ufuasi. Wakifanya hivyo watakuwa wakivunja sheria za uchaguzi. Watumishi wa umma hawafai kutumia afisi zao kuendeleza masilahi yao ya kisiasa.

Ni kwa misingi hii ambapo naunga mkono onyo lililotolewa juzi na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kwa watumishi wa umma ambao wameanza kampeni za mapema, ikitisha kuwanyima vyeti vya kuwaidhinisha kushiriki uchaguzi ujao.

Kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Twalib Mbarak, watumishi wa umma ambao wanataka kuanza kampeni za mapema wanapasa kujiuzulu mara moja hata kabla ya Februari mwaka ujao.

Lakini kando na kutoa onyo kama hilo, nadhani ingekuwa bora ikiwa EACC ingewataja hadharani watumishi hao ambao wameanza kampeni za mapema kinyume cha sheria.

Naamini Bw Mbarak na maafisa wake katika pembe zote za nchini wanawafahamu watumishi wa umma ambao tayari wameanza kujipigia debe wakitaka viti fulani kabla ya muda uliowekwa kisheria.

Kwa mfano, kuna maafisa wawili wa umma, mmoja anayemezea mate kiti cha ugavana wa Trans Nzoia na mwingine anayetaka kiti cha ugavana wa Siaya, ambao tayari wameanza kampeni za kujipigia debe ilhali hawajajiuzulu. Wengine wamekuwa wakifanya kampeni za kichinichini katika hafla za mazishi, makanisani na majukwaa mengine pasina kujali kuwa wao ni watumishi wa umma ambao hawapaswi kujihusisha na siasa.

Ndiposa EACC inafaa kuwataja hadharani wahusika kama hawa ili iwe funzo kwa wengine. Itakumbukwa mapema mwaka huu, Bw Mbarak alinukuliwa akisema sakata nyingi za ufisadi na aina nyingine za wizi wa fedha za umma katika serikali kuu na zile za kaunti hutokea nyakati kama hizi uchaguzi mkuu unapokaribia.

Alidai wahusika wakuu katika sakata hizo huwa ni maafisa wa umma, katika ngazi za serikali kuu na serikali za kaunti, wenye ndoto za kuwania viti vya kisiasa katika uchaguzi mkuu. Kulingana na Bw Mbarak, maafisa kama hao huingiwa na mshawasha wa kuiba fedha za umma ili kufadhili kampeni zao. Hii ni kutokana na ukweli wapiga kura wengi nchini, wenye uelewa finyu, huwachangamkia zaidi wanasiasa wanaowapa fedha na zawadi nyingine.

Kuna uwezekano mkubwa maafisa kadhawameanza kampeni za mapema wakitumia fedha na rasilimali za serikali kuendelea masilahi yao ya kisiasa.

You can share this post!

MATHEKA: Miungano mipya ya kisiasa isiwe ya kupiganisha raia

Mlipuko Beirut mwaka 2020 wasababishia raia umaskini