Makala

WASONGA: Idara ya Magereza ilinde hadhi na maisha ya wafungwa

March 10th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KENYA inapongezwa kama taifa lililo na Katiba inayotetea haki za watu wa matabaka yote, wakiwemo wafungwa.

Vilevile, taifa hili limetia saini mikataba mbalimbali ambayo kwa kiwango kikubwa inaoana na Sura ya Nne ya Katiba inayoangazia haki mbalimbali.

Lakini licha ya katiba ya sasa kuyapa uzito masuala ya haki, vitendo vya ukiukaji haki vimeendelea kushuhudiwa katika magereza yetu, kupitia kukithiri kwa mateso na mauaji tata ya wafungwa.

Ninadhani hii ndiyo maana mnamo 2017 Kenya ilipitisha sheria mahsusi ya kuzuia aina mbalimbali za mateso nchini Kenya. Sheria hii hutoa mwongozo wa kuzingatiwa kuzuia mateso, unyanyasaji na ukatili dhidi ya watu katika maeneo mbalimbali, yakiwemo magereza.

Lakini inasikitisha kuwa licha ya hayo, takwimu za hivi punde zilizotolewa na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNHRC) na shirika la kutetea haki, Amnesty International zinaonyesha kuwa kwa wastani zaidi ya visa 800 vya mateso vimeripotiwa katika magereza ya Kenya na vituo vya polisi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Na wengi wa wafungwa wanaopitia aina mbalimbali ya mateso wameishia kufariki. Hii ndiyo maana kifo kilichotokea majuzi katika gereza la Wanawake la Lang’ata, Nairobi, ni ishara kwamba wafungwa hawako salama katika baadhi ya magereza ya humu nchini.

Kwa mujibu wa usimamizi wa gereza hilo, Fatthiya Nassir, 41 aliugua maradhi yasiyojulikana na akakimbizwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) ambako iliripotiwa kuwa alifariki.

Lakini kinachoibua maswali ni kwamba ripoti ya upasuaji uliofanyiwa maiti yake inatoa ufichuzi tofauti. Kwamba mwendazake aligongwa kwa kifaa butu kichwani na katika shavu lake.

Kwa hivyo, kulingana na wanapatholojia, kuna uwezekano mkubwa kwamba Nassir aliuawa.

Sasa swali ni je, aliuawa na nani na kwa sababu gani? Na je, kitendo hicho kilitekelezwa vipi katika taasisi hiyo iliyo chini ya ulinzi mkali nyakati zote?

Kisa hiki ni sehemu ya visa vingi vya kuchukiza, nilivyorejelea hapa, ambavyo hutoa taswira ya magereza kama vyumba vya mateso; ambako wafungwa wanadhulumiwa na askari jela watundu au magenge ya wahalifu wanaotumikia vifungo humo.

Kisa kingine kiliripotiwa hivi majuzi katika gereza lenye ulinzi mkali la Naivasha ambako mfungwa Simon Nduro aliyedaiwa kuuawa baada ya kushambuliwa na walinzi wanane.

Vifo vya Nassir na Nduro, na vingine ambayo havijaripotiwa katika vyombo vya habari, bila shaka ni pigo kwa mageuzi ambayo yamefikiwa kwa dhamira ya kugeuza magereza na rumande kuwa asasi salama.

Ama kwa hakika wajibu mkuu wa idara ya magereza ni kuhakikisha kuna mazingira faafu kwa wafungwa kuweza kujirekebisha kimienendo na kisha waurejee katika jamii kama watu waadilifu.