Makala

WASONGA: Itakuwa kibarua sasa kwa kaunti kuzuia maambukizi zaidi

July 9th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya serikali ya kulegeza baadhi ya masharti ya kudhibiti kusambaa kwa virus vya corona sasa inatwika wajibu mkubwa wa kukabiliana na ongezeko la maambukizi kwa kaunti.

Hii ni kutokana na hali kwamba, watu wengi watakuwa wakisafiri kutoka miji mikubwa kama Nairobi na Mombasa hadi mashambani.

Na kaunti za Nairobi na Mombasa ndizo zinaongoza kwa idadi ya maambukizi, kulingana na takwimu za Wizara ya Afya za kila siku tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kilipogunduliwa nchini.

Wakazi wa kaunti hizo sasa watakuwa wakielekea mashambani kutokana na maisha magumu baada ya kupoteza ajira kufuatia makali ya janga hili.

Lakini kuna hatari ya watu hawa kusafirisha virusi vya corona hadi mashinani, kwani kuna waathiriwa wengi wasioonyesha dalili za ugonjwa huu.

Na kwa kuwa wataalamu wamethibitisha kuwa wagonjwa kama hawa wanaweza kusambaza virusi hivyo, kuna hatari ya wao kueneza ugonjwa huu kwa wazee na watu wenye magonjwa sugu kule mashinani.

Kwa hivyo, serikali zote 47 za kaunti zitahitaji kujiandaa kikamilifu kukabiliana na ongezeko la idadi ya wagonjwa watakaohitaji kuhudumiwa katika vituo maalum vya afya.

Zinahitaji idadi tosha ya vitanda maalum vya kuwatunza wagonjwa wa Covid-19, wahudumu wengi wa afya waliopewa mafunzo maalum, vifaa vya kusaidia wagonjwa kupumua (ventilators) na hifadhi ya hewa ya oksijeni na mahitaji mengineyo.

Lakini ingawa Rais Uhuru Kenyatta alitoa matakaa ya siku 30 kwa kaunti zote kuhakikisha zimeweka angalau vitanda 300 maalum vya kuwahudumia wagonjwa wa Covid-19, mnamo Juni 6, 2020, kaunti nyingi hazijatimiza agizo hilo.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya aliungama kuwa kufikia Julai 7, 2020 ni kaunti 16 pekee zilikuwa zimeweka angalau vitanda 300 katika vituo maalum vya kuwatenga wagonjwa hao.

Hii ni licha ya kwamba, Serikali Kuu ilizipa kaunti hizi Sh5 bilioni mnamo Mei kupiga jeki mipango yao kujiandaa kukabiliana na Covid-19.

Vile vile, kaunti hizo zilipokea Sh11 bilioni kutoka kwa wafadhili mbalimbali kutoka ng’ambo kwa sababu hizo hizo.

Na Ijumaa iliyopita, iliripotiwa kuwa kaunti hizi zilipokea ufadhili mwingine wa kima cha Sh6 bilioni kutoka kwa Shirika la Kenya Development Support Programme kufadhili mikakati ya kupambana na janga hili.

Fedha hizi ni kando na zile ambazo kila kaunti hutenga kutoka kwa bajeti zao kwa idara za afya.Kwa hivyo, zile kaunti ambazo hazijaanda wadi maalum zenye angalau vitanda 300 huenda ziliruhusu ufisadi kupenyeza katika mipango yake ya kukabiliana na janga hilo.

Kaunti zinafaa kuhakikisha pesa ambazo zilipokea kwa ajili ya mpango wa kukabiliana na Covid-19 zinatumika kwa shughuli zilizokusudiwa wala haziingii kwenye mifuko ya maafisa wachache.

Japo Rais Kenyatta ametangaza kuwa kila Mkenya anapasa kujitwika wajibu wa kuzuia kuenea kwa viruasi vya corona, mwenendo wa baadhi yao kupuuza masharti yaliyowekwa huenda ukataharisha maisha ya wengi mashambani.