Makala

WASONGA: Kenya ifanye kazi na atakayeibuka mshindi Amerika

November 3rd, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WAAMERIKA wanaelekea debeni leo Jumanne kumchagua Rais atakayewaongoza kwa miaka minne ijayo.

Wapigakura wataamua ni nani bora kati ya Rais wa sasa Donald Trump na mpinzani wake mkuu Joe Biden wa chama cha Democrat.

Kenya na Wakenya wamekuwa wakifuatilia uchaguzi huu kwa makini kwa sababu Amerika ni taifa tajiri na lenye nguvu zaidi duniani. Kwa miaka mingi, Amerika imekuwa mshirika wa Kenya katika masuala mbalimbali kama biashara na usalama, hususan, vita dhidi ya ugaidi nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Katika nyanja ya biashara, mnamo 2018, Kenya iliuza bidhaa za thamani ya Sh41 bilioni nchini Amerika chini ya mpango wa kustawisha mataifa ya Afrika Kibiashara (AGOA) ulioanzishwa mnamo 2000 chini ya utawala wa aliyekuwa Rais wa Amerika Bill Clinton.

Mapema mwaka huu 2020 Rais Uhuru Kenyatta alianzisha mazungumzo mapya na Rais Trump kuhusu uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na Amerika alipomtembelea Ikulu ya White House Februari 2020.

Hiyo ilikuwa ziara ya pili ya Rais Kenyatta nchini Amerika baada ya ile kwanza ya Agosti 2018.

Lakini tangu Trump aingie mamlakani baada ya kushinda uchaguzi mnamo Novemba, 2016, utawala wake haujakuwa na uhusiano mzuri na mataifa ya Afrika na watu weusi kwa ujumla.

Ametumia sera yake ya “Amerika Kwanza” kupunguza uhusiano kati ya utawala wake na Afrika pamoja na kuzuia wakimbizi kutoka bara hili (haswa mataifa ya kiislamu) kuingia Amerika. Aidha amekuwa akitumia lugha chafu kurejelea mataifa fulani ya Afrika.

Licha ya hayo, inatarajiwa kuwa ushindi wa Trump katika uchaguzi wa leo Jumanne utatoa nafasi ya kufanikishwa kwa mkataba wa kibiashara kati ya Amerika na Kenya.

Chini ya mpango huo wawekezaji kutoka Amerika wanatarajiwa kuanzisha biashara nchini Kenya, hatua ambayo imesawiriwa kuwa tishio kwa mpango wa kuanzishwa kwa eneo la biashara huru barani Afrika -Africa Continental Free Trade Area-AFCFTA.

Lakini Kenya isivunjike moyo endapo Biden ataibuka mshindi kwa misingi kwamba haifahamu sera zake kuhusu Afrika, na haswa taifa la Kenya.

Naamini kuwa hakuna Rais wa Amerika anaweza kupuuza Kenya katika mipango na sera zake za kigeni, kwa sababu taifa hili ni nguzo kuu katika mipango ya Amerika ya kupambana na ugaidi katika ukanda huu.

Kando na hayo Kenya ni mdhamini mkuu wa mchakato wa amani nchini Sudan Kusini na eneo zima la Maziwa Makuu ambako Amerika imekuwa ikiendeleza maslahi yake (ya kusaka soko kwa bidhaa zake).

Kwa hivyo, Kenya iwe tayari kufanyakazi na kiongozi yeyote ambaye Waamerika wataamua kuchagua leo kwa manufaa ya raia wa mataifa hayo mawili.