Makala

WASONGA: Machifu wasikwamishe mpango wa usafi mitaani

May 18th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SINA shaka kwamba Rais Uhuru Kenyatta alikuwa na nia njema alipoanzisha Mpango wa Kitaifa wa Usafi unaotekelezwa na mamia ya vijana katika mitaa ya mabanda mijini.

Mpango huo ulizinduliwa Aprili 25 katika kaunti saba zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa wa Covid-19 na unatarajiwa kuendelea kwa siku 30.

Dhima kuu ya mpango huu, alivyosema Rais, ni kuwapunguzia vijana makali yanayosababishwa na janga hili, ikizingatiwa kuwa wengi wao hawana ajira.

Na sasa, inasikitisha maafisa wa serikali waliotwikwa wajibu wa kusimamia mpango huu kaunti za Nairobi na Mombasa hawatekelezi majukumu yao ipasavyo.

Wiki jana, vijana walioajiriwa kufanya usafi katika mtaa wa Kibera waliandamana kwa kutolipwa tangu waajiriwe.

Waliekeza kidole cha lawama kwa machifu wa eneo hilo wakidai wanalenga kuwalaghai na kutia mfukoni pesa zao.

Maandamano sawia ya vijana yalitokea eneo bunge la Mvita, Mombasa makundi ya vijana wakilalamika kutolipwa walivyoahidiwa walipokuwa wakiajiriwa. Wao pia walielekeza mishale ya lawama kwa machifu na manaibu wao.

Naamini Rais alipotangaza kuanzishwa kwa mpango huu, tayari serikali ilikuwa imetanga fedha za kuwalipa.

Je, kwa nini baadhi ya machifu hawalipi vijana hawa ujira wao kwa wakati ilivyopangwa na serikali?

Ikiwa malalamishi yamechipuza katika kaunti za Nairobi na Mombasa huenda hali ni mbaya zaidi katika miji mingine ambako vijana sio jasiri kama wenzao katika miji hiyo miwili.

Ni makosa kwa maafisa wa serikali kuiharibia sifa kwa kuonekana kutozingatia maadili katika utendakazi wao.

Na machifu, ambao ndio “macho na masikio” ya Rais, na serikali yake, katika ngazi ya mashinani, ndio wamekuwa wakilaumiwa kwa kutosimamia ipasavyo mipango inayolenga kuwafaa wanajamii mashinani.

Kumeripotiwa visa vingi ambapo machifu wamepatika na kosa la kuuza chakula cha msaada iliyotolewa na serikali kwa ajili ya kusambaziwa wahanga wa njaa.

Na mwezi jana, vyombo vya habari viliripoti visa kadha ambapo machifu walilaumiwa kwa kusajili jamaa na marafiki zao katika mpango wa serikali wa kuwafaa wakongwe, mayatima na walemavu kwa fedha za matumizi kuzuia makali ya janga la corona.

Ilidaiwa machifu katika vitongoji duni vya Kibera, Mathare, Korogocho miongoni mwa vingine Nairobi waliwasajili watu wengine ambao hawastahiki kupata msaada huo.

Mwanamume mmoja aliiambia runinga moja ya humu nchini kwamba, baadhi ya wazee ambao majina yao yameorodheshwa kupewa fedha katika kitongoji cha Katwekera, eneo bunge la Kibra, ni wamiliki wa nyumba za kukodisha.

Hii ina maana wengi wa walengwa wa mpango huu wamekosa kufaidi kutokana na ruzuku hiyo ya Sh2,000 kila mwezi kutoka kwa serikali.

Serikali inapasa kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia vitendo vya utovu wa maadili kuingizwa katika mipango ya kuwafaa wanajamii kutokana na makali ya Covid-19.