MakalaSiasa

WASONGA: Madiwani wasisikize vilio vya wabunge kuhusu 'Punguza Mizigo'

July 23rd, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

NI ukweli ulio bayana kwamba katiba ya sasa imebuni nyadhifa nyingi, haswa za uwakilishi, ambazo ni mzigo kwa mlipa ushuru.

Hii ni ndiyo sababu miaka tisa baada ya katiba hii kuzinduliwa kumekuwa na miito ya mageuzi ili kupunguza gharama.

Rais Uhuru Kenyatta mwenye amenukuliwa mara si moja akilalamikia gharama ya juu ya ulipaji mishahara ya watumishi wa umma ambao unakadiriwa kutimu Sh560 bilioni kwa mwaka.

Hii ndio maana mnamo Julai 2017 aliunga mkono hatua ya Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu ya Watumishi wa Umma (SRC) kupunguza mishahara ya Maafisa Wakuu wa Serikali wakiwemo wabunge.

Kwa mantiki hii, pendekezo la mswada wa “Punguza Mizigo” kwamba idadi ya wabunge na maseneta ipunguzwe kutoka 416 hadi 147 lina mashiko.

Na inaridhisha kuwa kulingana na mswada huo, unaodhaminiwa na chama cha Thirdway Alliance, hatua hii itakupunguza gharama ya kuendesha asasi ya bunge kutoka Sh38.8 bilioni hadi Sh5 bilioni.

Hebu tafakari hayo ndugu msomaji, taifa la India lenye watu 1.2 bilioni lina wabunge 543 katika bunge lake la kitaifa. Lakini Kenya yenye takriban watu milioni 45 pekee ina jumla ya wabunge 349.

Kwa hivyo, ni wazi kwamba Kenya ina uwakilishi mkubwa ikilinganishwa na India yenye watu wengi na uchumi mkubwa.

Kwa msingi huu, mtizamo wangu ni kwamba mswada huu ambao sasa umekwisha wasilishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni mzuri kwa njia tatu kuu.

Kwanza unapunguza mzigo sio kwa misingi ya mishahara na marupurupu ya juu ambayo hulipwa wabunge bali ni kutokana na mchango wao kwa uchumi wa nchini.

Ukweli ni kwamba, mathalan, kati ya wabunge 349 na maseneta 67, ni wachache zaidi huchangia miswada, hoja na mijadala yenye manufaa kwa umma, jinsi ilivyodhihirishwa majuzi kwenye ripoti ya Shirika la Mzalendo Trust.

Pili, chama cha Thirdway Alliance kinachoongozwa na wakili Ekuru Aukot kimependekeza kwamba mgao wa fedha kwa serikali za kaunti uongezwe kama njia ya kupiga jeki ugatuzi. Kinataka angalau asilimia 35 ya mapato ya kitaifa yagatuliwe huku kitovu cha maendeleo kikiwa ngazi ya wadi wala sio maeneo bunge.

Tatu, mswada wa Bw Aukot unatoa pendekezo kuhusu namna na kupambana na ufisadi kwa kupendekeza kuwa muda wa kushughulikiwa kwa kesi hizo upunguzwe hadi siku 30.

Ama kwa hakika uovu huu, kulingana na takwimu ambazo zimetolewa na asasi mbalimbali za umma, huchangia taifa hili kupoteza takriban Sh600 bilioni kila mwaka, fedha ambazo zinaweza kuwekezwa katika miradi ya maendeleo.

Kwa hivyo, ni muhimu kwa madiwani kuchambua mswada huu kwa makini. Wasiyumbishwe na siasa zinazoibuliwa na wabunge wa ngazi kitaifa ambao tayari wanaupinga, hata kabla ya kuusoma.

Mustakabali wa taifa hili sasa uko mikononi mwa mabunge hayo 47, ikizingatiwa kuwa ni mabunge 24 pekee yanahitajika kuupitisha mswada huo na bila shaka utawasilishwa kwa Wakenya katika kura ya maamuzi licha ya pingamizi, haswa kutoka Bunge la Kitaifa.