Makala

WASONGA: Mapendekezo ya Aukot yashirikishwe katika BBI

October 22nd, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

JOPOKAZI la Maridhiano (BBI) linatarajiwa kuwasilisha ripoti yake kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wakati wowote wiki hii.

Hatua hiyo inajiri wiki moja baada ya kuangushwa kwa mswada wa mageuzi ya katiba, maarufu kama Punguza Mizigo, uliodhaminiwa na chama cha Thirdways Alliance chake wakili Ekuru Aukot.

Mswada huo sasa umezimwa kabisa kwa sababu kisheria ulihitaji kupitishwa na angalau mabunge 24 kati ya 47 ili uweze kufikishwa katika Bunge la Taifa na Seneti.

Bw Aukot anadai kuwa mswada huo haukuangushwa kwa sababu ulisheheni mapendekezo mabaya. Lakini, kulingana naye, ulifeli kutokana na “siasa mbaya” zilizoendeshwa dhidi yake na vigogo wa kisiasa nchini pamoja na madiwani kuhongwa.

Japo ni kweli mswada huo ulifeli kwa sababu wanasiasa wakuu nchini waliendesha kampeni chafu dhidi yake, Aukot hajatoa ushahidi kuhimili madai yake kwamba madiwani wa mabunge 31 walihongwa kusudi waukatae.

Lakini wito wangu kwa wote waliopinga mswada wa Punguza Mizigo ni kwamba kuna baadhi ya mapendekezo yake ambayo yanaweza kulifaidi taifa hili sasa na siku zijazo. Kwa hivyo, yawasilishwe sambamba na ripoti ya BBI bungeni kwa mjadala wa kina.

Mfano mzuri ni pendekezo kwamba muda maalum uwekwe wa kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi za ufisadi.

Japo muda wa siku 30 ulipendekezwa katika mswada wa Aukot ni mfupi mno, nadhani muda huo unaweza kuongezwa hadi miezi sita endapo Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) itapewa rasilimali zaidi kupambana na jinamizi hili.

Kujivuta kwa kesi za ufisadi kwa miaka mingi mahakamani ndiko kumelemaza vita dhidi ya uovu huo ambao ni mojawapo ya masuala tisa ambayo Rais Kenyatta na Bw Odinga waliazimia kukabiliana nayo chini ya mwavuli wa handisheki.

Ukweli ni kwamba kesi za ufisadi zinapoendeshwa kwa mwendo wa kinyonga, baadhi ya washukiwa hupata nafasi ya kuvuruga ushahidi.

Viongozi wanafaa kuelewa kuwa taifa jirani la Rwanda limepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya ufisadi kwa sababu mfumo wa kisheria umewekwa wa kuharikisha kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi zinazohusiana na uovu huu.

Kuiga China

Taifa hili pia linaweza kuiga mfano wa China ambako wale wanaopatikana na hatia ya kuiba pesa za umma hupewa adhabu kali kama ile ya kifo.

Sidhani kama taifa hilo lingepiga hatua kimaendeleo kiasi cha kuweza kuipa Kenya mikopo ya mabilioni ya fedha kila mara endapo haingeanzisha sheria kali ya kupambana na wizi wa pesa za umma.

Inakisiwa kuwa ufisadi hufyonza zaidi ya Sh700 bilioni katika sekta ya umma nchini kila mwaka.

Ni baada ya kudhibitiwa kwa ufisadi ambapo pendekezo la kuongezwa kwa mgao wa fedha kwa kaunti unaoungwa mkono na Bw Aukot,

Bw Odinga, maseneta na magavana, utapata mashiko. Vile vile, pendekezo la Bw Aukot kwamba baadhi ya mawaziri wateuliwe kutoka miongoni mwa wabunge pia halipasi kutupwa.

Hatua hiyo itaimarisha utendakazi na ushirikiano kati ya bunge la serikali kuu. Pendekezo hili lijadiliwe pamoja na ripoti ya BBI.