WASONGA: Matiang’i na Kibicho watoe majibu kuhusu Huduma Namba

WASONGA: Matiang’i na Kibicho watoe majibu kuhusu Huduma Namba

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI ilipoanzisha mpango wa kitaifa wa kusajili taarifa za Wakenya katika mfumo wa kidijitali (NIIMS) almaarufu Huduma Namba, mwaka jana, baadhi ya Wakenya waliibua mashaka kuuhusu.

Viongozi fulani wa kidini waliwaonya waumini dhidi ya kujisajili wakifananisha nambari hiyo na ile ya kishetani ya 666 inayorejelewa katika Biblia, kwenye kitabu cha Ufunuo.

Baadhi ya watu nao walidai kuwa serikali ilikuwa ikilenga kukusanya sampuli za DNA za watu kwa malengo fiche kama vile kuwafichua wanaume ambao wamepata watoto nje ya ndoa.

Lakini Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, walipuuzilia mbali nadharia hizo wakizitaji kama za kupotosha na zilizolenga kuhujumu mpango huo.

Walishikilia kuwa Huduma Namba inalenga kuwawezesha Wakenya kupata huduma za serikali kwa urahisi.

Waliongeza kuwa kupitia mpango huo serikali ililenga kudhibiti visa vya ulaghai vinavyoendeshwa na wakora ambao hughushi stakabadhi muhimu kama vitambulisho vya kitaifa.

Lakini ajabu ni kwamba zaidi ya mwaka mmoja baada ya awamu ya kwanza ya usajili huo, uliogharimu Sh8 bilioni pesa za umma, kukamilika, Wakenya 37 milioni waliosajiliwa hawajapewa kadi za Huduma Namba.

Maelezo ya Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho kwamba serikali ingali ‘‘inasafisha’ taarifa zilizokusanywa kutoka kwa Wakenya na kwamba kadi hizo zitaanza kutolewa Desemba’, hayaridhishi hata chembe.

Nashuku kuna siri fulani serikali inaficha katika mpango huu.

Swali ni je, mbona data zilizokusanywa kutoka kwa Wakenya katika awamu ya kwanza ya usajili inasafishwa kwa zaidi ya mwaka mmoja?

Mbona serikali inajiandaa kuanza awamu ya pili ya usajili wa Huduma Namba kwa gharama ya Sh10 bilioni kabla ya kutoa kadi kwa waliosajiliwa mwaka jana?

Serikali inafaa kutoa majibu ya maswali haya pamoja na mengine mengi ambayo wabunge wa mrengo wa Tangatanga wameuliza ili kurejesha imani ya Wakenya kwa mpango huo.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i pia anafaa kuitaja kampuni ya humu nchini ambayo wizara yake inadai ndiyo iliyopewa zabuni ya kuendesha awamu ya pili ya usajili wa Huduma Namba.

Maelezo kuhusu zabuni hiyo pia yawekwe wazi katika mtandao wa serikali, alivyoagiza Rais Kenyatta juzi baada ya kulipuka kwa sakata ya ufisadi katika mamlaka ya ununuzi wa dawa nchini (KEMSA).

Serikali ichukulie madai ya wabunge hawa wa Tangatanga kwa uzito kwani yanaweza kusababisha ghasia nchini kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

cwasonga@ke.nationmedia.com

You can share this post!

ONYANGO: Raila anavyochangia umaarufu wa Ruto kuongezeka

Muethiopia Lemlem aonyesha kinadada Wakenya kivumbi mbio za...