Makala

WASONGA: Rais akome kuzomea mawaziri hadharani

April 3rd, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

INASEMEKANA kuwa Rais wa kwanza nchini Hayati Mzee Jomo Kenyatta nyakati fulani angepandwa na hasira na kuwacharaza kwa bakora baadhi ya mawaziri wake kwa kutozingatia maagizo yake.

Na wakati fulani alimzomea hadharani aliyekuwa makamu wake Jaramogi Oginga Odinga walipotofautiana kuhusiana na masuala fulani ya uongozi na kisiasa. Matokeo ya mgongano huo yalikuwa ni kuondolewa kwa Bw Odinga katika cheo cha naibu mwenyekiti wa KANU na hatimaye kupokonywa wadhifa wa makamu rais. Mengine ni historia.

Natoa kumbukumbu hii ili kuonyesha ukuruba ulioko kati ya hulka za Mzee Kenyatta na mwanawe, Rais wa sasa, Uhuru Kenyatta.

Narejelea huu mwenendo wa Rais Kenyatta wa kuwazomea, kuwadunisha na kuwaabisha mawaziri wake hadharani kana kwamba ni wafanyakazi katika shamba lake. Hata wafanyakazi wa shambani wanafaa kuheshimiwa.

Kuna video ambayo majuzi ilisambazwa mitandaoni, ambapo Rais Kenyatta anaonekana akimzomea Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri alipokutana na Wakenya wanaoishi nchini Namibia katika mkahawa mmoja jijini Windhoek: “…. wewe Kiunjuri unakaa tu bila kuandika yale hawa Wakenya wanasema. Ama hayana manufaa kwako kwa sababu wewe ni Waziri wa Kilimo? Basi ulikuja kufanya kazi gani hapa?” Rais Kenyatta anasikika akisema kwa sauti ya juu.

Vile vile, alimkaripia Waziri wa Masuala ya Kigeni, Monica Juma kuhusiana na changamoto zinazowakumba Wakenya wanaoishi nchi za kigeni wanapotafuta paspoti za kisasa.

Mwaka jana Rais Kenyatta aligombeza Waziri Kiunjuri hadharani alipoongoza hafla ya ufunguzi wa Maonyesho ya Kimaitaifa ya Kibiashara ya Nairobi kuhusiana na sakata ya malipo ya Sh1.9 bilioni kwa wafanyabiashara badala ya wakulima waliowasilisha mahindi kwa maghala ya Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB).

Huku akionekana mwenye hamaki, Rais alimnyooshea kidole Bw Kiunjuri huku akifoka maneno makali kwa lugha ya Kikuyu akionekana kumwonya dhidi ya kuwalipa wafanyabiashara pesa ambazo zilinuiwa kulipwa wakulima halisi wa mahindi waliowasilisha mahindi yaoo mnamo 2017.

Rais Kenyatta anafaa kubadili mtindo huu wa kuonyesha ghadhabu zake kwa mawaziri wanaohudumu katika serikali yake. Hafai kuwadhalilisha kwa kuwazomea hadharani kila mara anapokasirishwa na utendakazi wao.

Hawa ni mawaziri ambao wanalipwa mishahara kutokana na kodi ambazo hulipwa na Wakenya bali sio pesa za Rais Kenyatta kama mtu binafsi. Ni wanaume na wanawake wenye familia zinazowathamini na kuwategemea kwa hali na mali. Isitoshe, wana marafiki wanaowaenzi.

Kile Rais anapasa kufanya anapohisi kutofurahishwa na mawaziri wake, ni kuwaita faraghani na kuwakanya dhidi ya hili na lile ambalo anahisi hawalifanyi inavyostahili.

Pili, badala ya kuonekana kila mara akiwazomea, hatua ya busara ni kuwaachisha kazi mara moja. Hii ni kwa sababu kipengee cha 152 cha Katiba ya sasa kimempa Rais mamlaka ya kuwateua na kuwapiga kalamu mawaziri bila kutafuta ushauri kutoka kwa mtu yeyote.