Makala

WASONGA: Rais apuuze wito wa kuzima usafiri msimu wa Krismasi

December 8th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WATAALAMU wamekubaliana kwamba virusi vya corona husambaa kwa kasi zaidi watu wanaposafiri kwingi kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Hii ndio maana baada ya mlipuko wa virusi hivyo nchini China, hatua ya kwanza iliyochukuliwa na taifa hilo pamoja na mataifa mengine ya ulimwengu ilikuwa ni kuzima safari za angani na ardhini kutoka na kuingia ndani ya mipaka yao.

Hatua hiyo pamoja na amri ya kutotoka nyakati za usiku, ziliathiri pakubwa chumi za mataifa hayo; haswa yale maskini kama vile Kenya.

Lakini kuanzia Septemba mwaka huu, mataifa mengi ya ulimwengu, yalianza kulegeza au kuondoa baadhi ya masharti hayo kwa lengo la kuokoa chumi zao.

Hata hivyo, Kenya na nchi za ulimwengu zimeendelea kuhimiza wananchi kuzingatia kanuni zingine za kuzuia msambao wa Covid-19 kama vile kuvalia barakoa, kutotangamana na kudumisha usafi wa mikono nyakati zote huku wananchi wakiruhusiwa kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.

Japo uchumi wa Kenya umeanza kufufuka tangu Septemba serikali ilipoondoa amri ya kuzima usafiri kutoka na kuingia kaunti zilizoathirika zaidi na ugonjwa huo, hali bado si shwari. Mapato ya serikali yamepungua kwa kiasi kikubwa ishara kwamba itachukua mrefu zaidi kwa uchumi kurejelea hali yake kabla ya mlipuko wa Covid-19.

Ni kwa msingi huu ambapo napinga vikali pendekezo la magavana kwamba Rais Uhuru Kenyatta arejeshe amri ya kuzima usafiri msimu huu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya ili kuzuia msambao wa corona.

Wanataka Rais azime usafiri kutoka na kuingia kaunti ambazo zinaendelea kuandikisha ongezeko la visa vya maambukizi kama vile Nairobi, Mombasa, Kiambu, Nakuru, Kajiado, Uasin Gishu, Busia, Machakos, Kisumu na Kilifi.

Wakiongozwa na mwenyekiti wao Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya wanadai kuingiwa na hofu kwamba huu msimu wa sherehe utachangia watu wengi kusafiri kutoka mijini hadi mashambani na kueneza maambukizi haswa miongoni mwa wakongwe.

Magavana hawa wanapasa kufahamu kwamba virusi vya corona tayari viko maeneo ya mashinani.

Visa vya maambukizi vinavyoshuhudiwa sasa havitokani na watu kusafiri kutoka maeneo ya mijini hadi mashambani, bali ni kwa sababu ya baadhi ya watu kupuuza kanuni za kimsingi.

Rais Kenyatta apuuzilie mbali wazo hili la magavana kwani watu wanahitaji kuendelea na shughuli zao za kuchuma hela wakati kama huu ambapo biashara nyingi hunoga watu wanaposafiri kwa wingi.

Wazazi na walimu pia wanafaa kujiandaa mapema kwa ufunguzi wa shule kuanzia Januari 4, 2021, hali ambayo haiwezi kufanyika ikiwa usafiri utadhibitiwa.