Makala

WASONGA: Rais atekeleze ushauri wa jopokazi na kufungua shule

September 22nd, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MDAHALO ambao umeshika kasi nchini kwa sasa unahusi ni lini shule zitafunguliwa baada ya kubainika kuwa maambukizi ya virusi vya corona yamepungua kwa kiwango kikubwa.

Kushuka kwa idadi ya maambukizi kumeamsha ari ya wanasiasa kurejelea mikutano ya hadhara hivyo kukiuka kanuni ya Wizara ya Afya ya watu kutotangamana ili kuzuia kueneo la virusi vya corona.

Serikali nayo imeanza kulegeza masharti kuhusu idadi ya watu wanaopaswa kuhudhuria mazishi na kujumuika katika maeneo ya ibada.

Hii inamaana kuwa hatari haipo tena kama awali, kwani baadhi ya wanaojumuika katika mikutano ya wanasiasa, hafla za mazishi na katika maeneo ya ibada ni wanafunzi ambao wamesalia nyumbani tangu Machi 15 shule zilipofungwa.

Kwa hivyo, wadau katika sekta ya elimu, wakiongozwa na Waziri wa Elimu George Magoha, wanafaa kuamua haraka kuhusu ni lini shule zitafunguliwa; kabla ya Januari 2021. Wanafaa kuwapa kipaumbele wanafunzi wa Darasa la Nane na wenzao wa Kidato cha Nne. Wale wengine wanaweza kurejelea mwaka ujao.

Maandalizi ya haraka yafanywe ili wanafunzi hawa ambao walitarajiwa kufanya mitihani ya KCPE na KCSE mwishoni mwa mwaka huu, warejee shuleni waendelea na masomo.

Itakuwa rahisi kwa watahiniwa hawa 1.8 milioni kuendelea na masomo wakizingatia kanuni za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Miundomsingi, haswa katika shule za umma, inatosha kuhakikisha watahiniwa wote wanaendelea na masomo yao pasina kusongamana madarasani. Hii ni kwa sababu watatumia madarasa ambayo hutumiwa na wanafunzi wa madarasa na vidato vya chini.

Katika mazingira kama hayo, serikali itaweza kuhakikisha wanapata barakoa, sanitaiza na maji kama njia ya kuhakikisha kuna usafi na wanafunzi hawaambukizani.

Kwa hivyo, pendekezo la kamati maalum iliyoteuliwa na Waziri kutathmini wakati mwafaka wa kufunguliwa kwa taasisi za elimu kwamba watahiniwa wa KCPE na KCSE waruhusiwe kurejea shuleni mnamo Oktoba 19, 2020 lina mashiko.

Serikali ikubaliane na wazo hilo ili wanafunzi hawa waandaliwe ndiposa waweze kufanya mitihani hiyo katikati mwa Aprili 2021. Hili linawezekana kwa sababu, kimsingi, ni asilimia ndogo zaidi ya maswali katika mitihani ya KCPE na KCSE hutahiniwa kutoka mitaala ya darasa la nane au kidato cha nne.

Rais Uhuru Kenyatta anafaa kuidhinisha pendekezo hili katika hotuba yake ijayo kwa taifa ili watahiniwa wasipoteze mwaka mzima wa masomo, hali ambayo itavuruga maisha yao ya baadaye.