MakalaSiasa

WASONGA: Rais Kenyatta akatae nyongeza ya mshahara wake

May 12th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MNAMO mwezi Machi mwaka huu Rais Uhuru Kenyatta aliunga mkono pendekezo la Tume ya Kukadiria Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC) ya kufutilia mbalimbali baadhi ya marupurupu ambayo watumishi wa umma hupokea.

Alisema hatua hiyo iliyotangazwa na mwenyekiti wa tume hiyo Lynne Mengich itaiwezesha serikali yake kufikia azma yake ya kupunguza mzigo wa kulipa mishahara kuelekeza pesa katika miradi ya maendeleo.

Na nakumbuka kwamba kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 Rais Kenyatta alitetea vikali hatua ya tume hii ya kupunguza mishahara ya wabunge na maafisa wengine wakuu serikali, akiwemo yeye na naibu wake.

Kwa mfano, mshahara wake ulipunguzwa kutoka Sh1,65 milioni hadi Sh1.44 milioni kila mwezi huku ule wa Naibu wake, William Ruto ukanyolewa kutoka Sh1.4 milioni hadi Sh1.23 milioni.

Mwenyekiti wa SRC, wakati huo, Bi Sarah Serem alisema upunguzaji wa mishahara ya watumishi wakuu wa serikali, japo ulipingwa na wabunge, kungeiwezesha serikali kukomboa Sh8 bilioni kila mwaka.

Rais Kenyatta alisema alikubaliana na kauli ya Serem kwamba Sh600 bilioni ambazo serikali hutumia kulipia mishahara na marupurupu ya watumishi wa umma kila mwezi ni juu mno na ndio maana serikali hukopa pesa za kufadhili miradi ya maendeleo kutoka ng’ambo.

Sasa swali langu ni je, mbona sasa Rais Kenyatta amenyamaza huku Wizara ya Fedha ikipanga kuongeza mshahara wake na wa Dkt Ruto kwa kima cha asilimia 3.9?

Mbona Rais hajasema lolote kuhusu hatua ya wabunge kujitengea marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mwezi licha ya pingamizi kutoka kwa Hazina Kuu na SRC?

Kulingana na makadirio ya bajeti ya kitaifa yaliyowasilishwa bunge wiki jana, bajeti ya pamoja ya mishahara ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto imeongezwa kutoka Sh36.6 milioni hadi Sh38 milioni kwa mwaka. Hii ina maana kuwa mshahara wa Rais utapanda hadi Sh1.7 milioni.

Hali hii inasikitisha kwa sababu huu ni wakati mgumu kwa nchi hii ambayo uchumi wake unazorota kila uchao huku mzigo wa madeni ukiendelea kupanda.

Japo serikali inasema kwamba hali ya uchumi ni shwari ukiwa unatarajiwa kukua zaidi mwaka huu, mwananchi wa kawaida angali anatatizika kwa kutozwa ushuru mkubwa huku serikali ikidinda kutoa nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi wa madaraja ya chini.

Namtaka Rais Kenyatta ajitokeze na kukataa nyongeza hiyo ya mshahara wake la sivyo huenda wananchi wakaanza maasi dhidi ya serikali yake.

[email protected]