WASONGA: Sensa ya mwaka huu iwe na uadilifu

WASONGA: Sensa ya mwaka huu iwe na uadilifu

Na CHARLES WASONGA

SHUGHULI ya kuhesabu watu mwaka huu ina umuhimu mkubwa kwa taifa hili.

Hii ni kwa sababu data itakayokusanywa itatumika kupanga mipango ya maendeleo nchini kwa mara ya kwanza chini ya utawala wa ugatuzi.

Pia zoezi hilo maarufu kama sensa linafanyika wakati ambapo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inahitaji takwimu itakazotumia kutathmini upya mipaka ya maeneo ya uwakilishi huku shinikizo za marekebisho ya Katiba kupitia kura ya maamuzi zikishika kasi.

Wakati huu, tume hiyo inakagua sahihi 1.4 milioni za wapiga kura zilizokusanywa na chama cha Thirdways Alliance, chini ya kauli mbiu, “Punguza Mzigo” kikitaka katiba ifanyiwe mageuzi ili kupunguza idadi ya wabunge na maseneta kutoka 416 hadi 147.

Chama hichi kinachoongozwa na Dkt Ekuru Aukot kinadai kuwa idadi ya sasa ya wawakilishi ni mzigo mkubwa kwa mlipa ushuru na uchumi kwa jumla.

Isitoshe, sensa ya mwaka huu, itakayofanyika Agosti 24 na 25, inajiri miezi michache baada ya Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) kupendekeza mfumo mpya wa ugavi wa pesa za maendeleo miongoni mwa kaunti unaoipa idadi ya watu uzito mkubwa zaidi.

Kulingana na mfumo huo, asilimia 45 ya fedha zitakazotengewa serikali za kaunti katika miaka mitatu ijayo zitagawanywa kwa misingi ya watu katika kaunti mbalimbali.

Hii ina maana kuwa kaunti zenye idadi kubwa ya watu zitapata mgao mkubwa wa fedha huku zile zenye watu wachache zikipata mgao mdogo.

Kwa msingi huu, wananchi pamoja na viongozi wa kisiasa watafuatilia sensa ya mwaka huu kwa makini zaidi. Nadhani hii ndio maana Shirika la Kataifa la Takwimu (KNBS) limeamua kutumia teknolojia ya kisasa kuendesha zoezi hilo, ambalo linakadiriwa litagharimu Sh18.5 bilioni, ili kuhakikisha kuwa matokeo yatakayopatikana ni sahihi.

Idadi kubwa ya watu wanaoajiriwa wakati huu kuendesha zoezi hilo ni wale ambao wanaweza kutumia mitambo 164,700 ya kieletroniki iliyonunuliwa na KNBS kwa ajili ya sensa ya mwaka huu.

Lakini shirika hilo halifai kukataa kitako na kutarajia kuwa matumizi ya mitambo hiyo ni hakikisho tosha la kupatikana kwa matokeo sahihi yanayoakisi idadi sahihi ya watu nchini, kimaeneo na kikabila.

Ushauri wangu kwa KNBS ni kwamba inapasa kuhakikisha kuwa mitambo itakayotumiwa, kwa mfano, katika shughuli za kukusanya, kutuma na kuchanganua data imefanyiwa majaribio na kubainika kuwa sawa kiutendakazi.

Maafisa wa shirika hili pia wahakikishe kuwa mitambo hiyo imetimiza viwango stahiki vya ubora ili isifeli jinsi ambavyo baadhi ya mitambo ya kieletroniki iliyotumiwa na IEBC katika chaguzi za miaka ya 2013 na 2017 ilifanya.

Muhimu zaidi ni kwamba KNBS inapasa kuhakikisha kuwa wahudumu watakaotumia mitambo hiyo wamepewa mafunzo tosha na wapigwe msasa kuhakikisha kuwa ni watu waadilifu na wazalendo.

KNBS pia ihakikishe kuwa sensa ya mwaka huu inasimamiwa vizuri ili kuzuia visa vya udanganyifu.

 

You can share this post!

ODONGO: Rivatex ichangie katika ufufuzi wa kilimo cha pamba

WANDERI: Madai ya njama ya kuua Ruto yasitiwe mzaha

adminleo