Makala

WASONGA: Tamaa hii ya walimu kuandaa masomo ya ziada ikome

April 5th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

Baada ya kisa cha kwanza cha maambukizi ya virusi vya corona kugunduliwa nchini, serikali iliagiza shule na taasisi za elimu ya juu kufungwa.

Sababu kuu iliyochangia hatua hii ni kwamba, ni rahisi kwa virusi hivyo kusambaa katika mazingira ya shule, haswa madarasani, kutokana na mtagusano kati ya walimu na wanafunzi.

Kwa hivyo, serikali iliwashauri wazazi wahakikishe watoto wao wanakaa nyumbani hadi wakati hatari hii itapungua na washauriwe kurejea shuleni.

Na ili kuhakikisha wanafunzi hawaathiriki zaidi kimasomo, Taasisi ya Kuandaa Mitaala Nchini (KICD) kwa ushirikiano na Shirika la Habari Nchini (KBC) inaendesha vipindi vya mafunzo ya ziada kupitia KBC Redio (idhaa za Kiswahili na Kiingereza) na runinga ya Edu TV. Vipindi vingine vya masomo pia vinaendeshwa kupitia mtandao wa YouTube.

Lakini inakera kuwa, kuna baadhi ya walimu wanaoendesha masomo ya ziada katika nyumba zao, kwa malipo, licha ya marufuku iliyowekwa na serikali kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19, kama ambavyo Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kilisema juzi.

Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Hesbon Otieno alisema kuwa, chama hicho kimepokea habari kwamba, baadhi ya walimu wanashawishiwa na wazazi wawafundishe watoto wao katika nyumba zao (walimu hao).

Ikiwa madai ya Bw Otieno ni kweli (ninavyoamini) basi walimu na wazazi wanaoshiriki njama hii wanahatarisha maisha yao na ya wanafunzi husika.

Hii ni kwa sababu, kwa kuendesha mafunzo katika mazingira kama hayo, ni vigumu kwa walimu husika kudumisha kanuni au hitaji la mtu kuwa umbali wa angalau mita moja na nusu kutoka kwa mwingine.

Kanuni hii imewekwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), na inasisitizwa kila siku na Wiziri wa Afya Mutahi Kagwe, kama njia mojawapo za kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huu hatari.

Walimu na wazazi wanaoshirikiana kufanikisha shughuli hii haramu wanafaa kuelewa wao ni sawa na wauaji ikizingatiwa kuwa kufikia sasa Covid- 19 imeua zaidi ya watu 53,000 duniani, wanne kati yao wakiwa ni Wakenya. Na zaidi ya watu milioni moja wameambukizwa virusi vya corona duniani, Kenya ikirekodi zaidi ya visa 100 kufikia sasa.

Wazazi ambao wanawapeleka watoto wakafunzwe katika nyumba za walimu wajue dhana kuwa Covid-19 inawaua wazee pekee au wale wenye magonjwa sugu, haina mashiko tena.

Hii ni kwa sababu juzi msichana mwenye umri wa miaka 12 alifariki kutokana na ugonjwa huo nchini Ubelgiji, sawa na mvulana mwenye umri wa miaka 13 nchini Uingereza.