MakalaSiasa

WASONGA: Tamko la Ruto ni hatari katika vita dhidi ya ufisadi

March 3rd, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

TANGU Rais Uhuru Kenyatta alipofanya mabadiliko ya uongozi katika Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODDP), vita dhidi ya ufisadi vinaonekana kuelekea kuzaa matunda.

Maafisa kadha wakuu serikalini wamekamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka mbalimbali ya ufisadi yaliyofichuliwa katika mashirika wanayosimamia.

Orodha ya maafisa hao ni ndefu na inajumuisha aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Lilian Omollo na Ken Tarus na Joe Sang’ waliokuwa wakurugenzi wakuu wa kampuni za Kenya Power na Kenya Pipeline, mtawalia.?Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto wamepongeza utendakazi wa DCI George Kinoti na mwenzake wa DPP Nordin Haji huku wakionya wanasiasa dhidi ya kuingiza siasa katika utendakazi wa maafisa hao.

Kulingana na wawili hao, asasi hizi mbili, sawa na idara ya mahakama, zinapasa kuruhusiwa kuendesha kazi zao katika mazingira huru bila kuingiliwa kwa njia yoyote ile.

Sasa kinaya ni kuwa Dkt Ruto ndiye yuko mstari wa mbele kuingilia utendakazi wa Bw Kinoti na maafisa wake kuhusiana na sakata ya hivi punde inayozingira ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kamwerer katika kaunti za Baringo na Elgeyo Marakwet, mtawalia.

Kwa mtazamo wangu, hatua ya Naibu Rais kupinga ripoti ya Bw Kinoti iliyosema kuwa serikali ilipoteza Sh21 bilioni katika kashfa hiyo ni sawa na kuingilia utendakazi wa asasi hiyo huru.

Na kauli yake kwamba ripoti ya Bw Kinoti ni “uwongo mtupu” ni kielelezo cha kudunisha ama kukosa imani na utendakazi wa afisa huyu ambaye aliteuliwa na bosi wake, Rais Kenyatta kufanya kazi kuchunguza, miongoni mwa mingine, kesi za ufisadi kwa manufaa ya Wakenya walipa ushuru.

Isitoshe, kauli ya Dkt Ruto yaonyesha wazi kwamba hamheshimu Rais huyu anayepania kumrithi mnamo 2022. Ukweli ni kwamba kauli ya Ruto ni hatari kwa vita dhidi ya ufisadi nchini kwa sababu huenda ikawafanya wananchi wa kawaida kushuku utendakazi wa afisi ya DCI.

Na kwa sababu Naibu Rais alitoa dai hilo ndani ya Mahakama ya Juu mbele ya Jaji Mkuu David Maraga na majaji wengi wa hadhi ya juu, ushahidi utakaokusanywa na DCI pia huenda ukatiliwa shaka mahakamani washukiwa wa sakata hiyo watakaposhtakiwa rasmi.

Kauli ya Dkt Ruto inaashiria kuwa kuna mengi anayofahamu kuhusu sakata hiyo au anajaribu kutumia nafasi yake serikalini kuwakinga washukiwa fulani kwa manufaa yake wala sio ya Wakenya.

Endapo ni kweli kwamba Naibu Rais anapania kuliongoza taifa hili kuanzia 2022, akome kuingilia vita dhidi ya zimwi hili la ufisadi.