Makala

WASONGA: Tufungulie watalii kutoka nchi za nje kwa uangalifu

July 30th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HUKU kukiwa na matumaini makubwa ya kufufuliwa kwa sekta ya utalii kufuatia kurejelewa kwa safari za ndege za kimataifa, wageni kutoka nje wawekewa masharti makali kuhakikisha walio na virusi vya corona wanazuiwa kuingia nchini.

Ingawa serikali ilitangaza kuwa wakataoruhusiwa kuingia nchini ni wasafiri wenye vyeti vya kuonyesha wamepimwa na kubainika hawana virusi vya corona, bado kuna changamoto.

Kwa mgeni kuonyesha cheti kama hicho sio thibitisho kuwa hana virusi hivyo. Mtu anaweza kuambukizwa ugonjwa huo siku chache baada ya kupokea cheti hicho kisha akapanga safari ya kuzuru Kenya.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba, mgeni kama huyo anaweza kutua katika Uwanja wa Kimataifa ya Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi au ule wa Moi (Mombasa) kabla ya kuanza kudhihirisha dalili za ugonjwa wa Covid-19 kama vile joto jingi mwilini. Kwa hivyo, vifaa vya kupima joto havitatambua kuwa mtu kama huyo ni mgonjwa.

Ikizingatiwa kuwa Waziri wa Uchukuzi James Macharia na mwenzake wa Utalii Najib Balala wametangaza kuwa wageni watakaotua nchini kutoka ng’ambo hawatahitajika kuwekwa karantini ya siku 14, kuna hatari kubwa ya aina fulani ya virusi vya corona kuingia nchini.

Tayari mashirika manne ya ndege za kimataifa yametangaza kuwa yako tayari kuanza safari zao za nje na ndani ya Kenya kuanzia Agosti 1. Mashirika hayo ni; British Airways, KLM, Air France na Qatar Airways na baadhi yao yatafanya safari mara nne kwa wiki.

Kwa kuwa baadhi ya wageni watakuwa wakitoka mataifa ambayo tayari yanashuhudia wimbi la pili la ongezeko la maambukizi, itakuwa rahisi kwa baadhi yao kuingiza virusi vya corona nchini kwani hawatahitajika kutengwa kwenye karantini kwa siku 14.

Hali kama hii, bila shaka, inahujumu juhudi zinazofanywa na serikali kudhibiti janga hilo ambalo limevuruga maisha ya Wakenya katika nyanja zote.

Itakumbukwa kuwa, kabla ya serikali kuzima safari za ndege za abiria kutoka mataifa ya nje kutua nchini baada ya ugonjwa huo kugunduliwa nchini kwa mara ya kwanza, kulikuwa na visa kadha vya watu walioingia nchini kupatikana na virusi vya corona siku chache baada ya kupitishwa katika uwanja wa JKIA. Kwa hivyo, kuanzia Agosti 1, serikali inapasa kuweka masharti makali kwa watu watakaowasili kutoka mataifa kama vile; Japan, Amerika, Uhispania, Uhispania miongoni mwa mengi ambayo yameshuhudia ongezeko la maambukizi katika siku za hivi karibuni.

Kwa mfano, serikali ianzishe mbinu ya kupimwa wageni na matokeo kutolewa papo kwa hapo katika viwanja vya ndege, badala ya kutegemea vifaa vya kupima joto. Mbinu kama hii, ingawa ni ghali, ni hitaji muhimu katika mpango mzima wa kufufua uchumi.

Inaeleweka kuwa serikali ina hamu kubwa ya kuona sekta ya utalii, iliyoathirika zaidi, ikifufuka. Hii ni baada ya takwimu kuonyesha sekta hiyo imepoteza mapato ya kima cha Sh80 bilioni tangu Machi mwaka huu.

Ingawa wamiliki wa hoteli nchini wamelalamika kuwa huenda watalii wakaogopa kuja nchini endapo watawekewa masharti makali kama vile hitaji la karantini, hiyo haimaanishi serikali iruhusu virusi zaidi kuiingia nchini. Kenya iige mfano wa Uingereza, China na jimbo la Hong Kongo kwa kuweka masharti makali kwa wageni watakaoingia humu.