Makala

WASONGA: Tusiumbue mahakama, ndio kimbilio letu la mwisho

March 24th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HALI ya wasiwasi imetanda nchini baada ya Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kufichua kuwa imepokea jumla ya malalamishi 15 dhidi ya majaji sita wa Mahakama ya Juu nchini, akiwemo Jaji Mkuu David Maraga.

Wengine ni; Njoki Ndung’u, Smokin Wanjala na Mohammed Ibrahim anayedaiwa kumtisha bawabu mmoja nyumbani kwake, japo kesi hiyo haijafikishwa katika JSC. Naye Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu anakabiliwa na tuhuma za ufisadi huku mchakato wa kumwondoa afisini Jaji Jackton Ojwang’ ukiwa umeanza.

Hii ina maana kuwa Jaji wa mahakama hiyo ambaye hagubikwi na shauku yoyote ni Isaac Lenaola. Isitoshe, JSC inasema imepokea malalamishi kadha dhidi ya baadhi ya majaji na mahakimu wa mahakama za chini.

Hali hii inaibua hofu kwa sababu, kimsingi, Idara ya Mahakama ndio asasi ambayo haipasi kulaumiwa kwa lolote. Maafisa wake hawafai kuhusishwa na makosa ya ukiukaji katiba na madili stahiki ndiposa maamuzi yao yaweze kuaminika.

Waama, mahakama ndio tegemeo la wananchi wanyonge ambao, aghalabu, hudhulumiwa na vitengo vingine vya utawala, kama vile, Afisi Kuu na Bunge. Ina maana kuwa asasi hii inapasa kuendeleza wajibu wake wa kufasiri sheria na kutatua kesi kwa njia huru, haki na itakayoaminiwa na wote.

Nasema hivyo kwa sababu, kutoaminika kwa majaji wa idara ya mahakama kunaweza kusababisha madhara makubwa zaidi nchini, jinsi ilivyodhihirika wakati wa mzozo wa kisiasa baada ya uchaguzi mkuu 2007.

Fujo, maafa na uharibifu wa mali yaliyoshuhudiwa nchini wakati huo yalichangiwa na hali kwamba Bw Raila Odinga na wafuasi wake, hawakupeleka malalamishi yao mahakamani kwa hofu kwamba, hawangepata haki.

Ni muhimu kutaja hapa kwamba, kando na hayo, ghasia hizo ziliathiri mwelekeo na mkondo wa siasa za taifa hili kwa kiwango kikubwa; kwa uzuri au kwa ubaya. Hii ni kwa sababu muungano wa kisiasa uliobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto, kimsingi, ulitokana na kesi zilizowakabili katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC) kwa kuhusishwa na ghasia hizo.

Kwa hivyo, JSC inapasa kuhakikisha uchunguzi dhidi ya majaji wa Mahakama ya Juu unaendeshwa kwa njia huru na haki ili kurejesha imani ya Wakenya kwa asasi hiyo na idara ya mahakama kwa ujumla.

Utawala wa sheria utanawiri tu nchini ikiwa wananchi wataamini kuwa mahakama zinaweza kutoa haki kwa haraka nyakati zote.