Makala

WASONGA: Utekelezaji duni wa sera umetatiza sekta ya madini

January 7th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KATIKA mwongo uliopita, kumekuwa na imani miongoni mwa wanasera kuwa mabadiliko ya kisheria ni nguzo kuu iwapo tunataka mageuzi yatakayoleta maendeleo katika nchi hii.

Lakini nguvukazi, ufadhili na kipaumbele hupewa mchakato wa kubadilisha sheria hizi huku mwisho wake ukitajwa kama mafanikio makuu kwa taifa.

Hata hivyo, mpango mzima wa utekelezaji wa mageuzi haya ya kisheria husahaulika baada ya sheria hizo kuchapishwa.

Ukosefu wa miundombinu ya kutosha katika utekelezaji hulemaza uwezo wa udhibiti wa kisheria maadamu ni kazi ambayo imeachiwa wizara husika.

Changamoto kuu katika baadhi ya sheria ni kuwa zinalenga kupunguza mamlaka ya wizara ambazo zimepewa jukumu la utekelezaji wa sheria hizo.

Kwa mfano, Sheria ya Madini ya 2016 ilipigiwa debe mno ikisemekana kuwa imetoa fursa mpya kwa Kenya kufufua sekta yake ya uchimbaji madini na kuchangia kukuza uchumi.

Baada ya kubadilisha sheria ya awali ili iwiane na Katiba ya sasa, sheria hiyo iliangazia baadhi ya mianya katika uongozi wa sekta hiyo.

Katika mapito ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki, leseni nyingi za kuchimba madini zilitolewa. Lakini waziri mpya aliyeingia 2013 alianza kwa kufuta leseni hizo.

Kufutiliwa mbali kwa lesni hizi kulisababisha Kenya kushtakiwa katika mataifa ya kigeni, kesi ambazo zilikuwa ghali mno kujitetea. Kwa mfano, kampuni ya Cortec ilitaka ifidiwe Sh200 bilioni kutokana na hilo.

Ni mambo haya ambayo yalichangia katika kubuniwa kwa Sheria ya Madini, mchakato mpya wa kutoa leseni, na Bodi ya Hatimiliki za Madini.

Ningependa kuzungumzia bodi hii ambayo ilipewa jukumu la kudhibiti hatimiliki za uchimbaji pamoja na kumshauri waziri husika.

Bodi hii imekuwa tu na kazi hewa kwani haina hata bajeti wala ufadhili wa kuhakikisha majukumu yake yemetekelezwa.

Naishangaa sana bodi hii kwa kukosa mwongozo kutoka kwa wizara wa kuonyesha maendeleo yake na maamuzi kuhusu madini. Hapa ndipo unafaa kutambua kuwa licha ya juhudi za mageuzi ya usimamizi, mambo yamesalia vile vile.

Si jambo la kushangaza kuwa licha ya kampuni nyingi kupewa leseni, bado hakuna uchimbaji unaoendelea nchini.

Suala linguine nyeti ambalo sheria hiyo ililenga kusuluhisha ni mzozo baina ya serikali kuu na serikali za kaunti ambapo mgao wa fedha kutokana na madini umekwamiza shughuli.

Miaka miwili baadaye, nashangaa kuwa Sheria ya Madini imekosa kufikia malengo yake. Ingawa nimeangazia sana kuhusu sheria yenyewe, ukweli ni kwamba imefeli kutokana na utekekelezaji duni.

Katika mwaka huu wa 2020, kuna fursa mpya ya kuhakikisha utekelezaji wa sheria zote umefanyika ili kutimiza ahadi ya sekta ya madini kukuza uchumi wa nchi na hatua isipochukuliwa, taifa litaumia zaidi.