Makala

WASONGA: Viongozi wa Kenya waige Mkapa, sio kumsifia pekee

July 28th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

VIONGOZI mbalimbali nchini wamemmiminia sifa aliyekuwa Rais wa Tanzania marehemu Benjamin William Mkapa wakimtaja kama kiongozi shupavu na mpatanishi mkubwa.

Wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, viongozi hao hasa wametaja mchango wa kiongozi huyo katika mchakato wa upatanisho uliozima ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007, ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa na zaidi ya wengine 650,000 wakaachwa bila makao.

Lakini litakuwa jambo la busara zaidi ikiwa viongozi hawa wataiga sifa hii ya marehemu Mkapa, anayezikwa kesho, kwa kupalilia maelewano miongoni mwao haswa wakati huu ambapo joto la siasa za uchaguzi mkuu wa 2022 linapoanza kupanda.

Itakuwa unafiki mkubwa ikiwa wanasiasa kama vile Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Moses Wetang’ula na Naibu Rais William Ruto hawataiga mfano wa Mkapa ili kusitokee ghasia zingine kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Kwa sababu viongozi hawa walitagusana kwa karibu zaidi na marehemu Mkapa walipohudumu kama wanachama wa Kamati ya Upatanishi wakiwakilisha mirengo yao, wanapasa kuwa walijifunza mengi kutoka kwa kiongozi huyo.

Dkt Ruto na Bw Mudavadi walikuwa miongoni mwa wawakilishi wa ODM katika meza hiyo ya mazungumzo huku Bw Wetang’ula akiwa mmoja wa wale waliowakilisha chama cha PNU ambacho Mzee Mwai Kibaki alikitumia kutetea kiti cha urais.

Kwa hivyo, kwa mfano, Dkt Ruto na Bw Odinga wanafaa kuwadhibiti wafuasi wao kuelekea uchaguzi mkuu ujao ili kusitokee mafarakano yeyote kwani watakaoumia ni wananchi wa kawaida.

Kwa upande wao, Mbw Mudavadi na Wetang’ula ambao sasa wanapambana na mrengo wa Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa wakiwania ubabe wa kisiasa magharibi mwa Kenya, wapalilie siasa za kuvumiliana.

Wote wafaa waboreshe siasa zao na wasifa wa marehemu Mkapa kama ishara ya heshima kwa kiongozi huyo ambaye aliheshimika sio tu nchini Tanzania bali barani Afrika na ulimwengu kwa ujumla.

Kwake Rais Kenyatta, sifa alizommiminia Mkapa hazitakuwa na maana yoyote ikiwa hataanzisha mchakato wa kupalilia maridhiano kati yake na Naibu Dkt Ruto.