Makala

WASONGA: Viongozi waheshimu kanuni za kuzuia corona

June 9th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI iliweka kanuni za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona tangu mwezi Machi 2020 ili kuokoa uchumi wa taifa hili kutokana na makali ya janga hili.

Kwa mfano, serikali ilipiga marufuku mikutano ya kisiasa na kijamii, ikaamuru baa, vilabu vya burudani na kumbi za fani mbalimbali za sanaa zifungwe ili kukomesha mtagusano wa watu.

Taasisi za elimu zilifungwa sawa na majumba ya ibada huku hafla za mazishi nazo zikitakiwa kuhudhuriwa na watu wasiozidi 15 pekee. Kanuni hizi, pamoja na zingine, zilipaswa kuzingatiwa na Wakenya wote pasi kujali hadhi yao, ikizingatiwa kuwa virusi vya corona, ambavyo husababisha ugonjwa wa Covid-19, havibagui mtu yeyote.

Lakini inavunja moyo kuona kwamba wapo viongozi wetu wa kisiasa na maafisa wakuu wa serikali ndio wamekuwa katika mstari wa mbele kukaidi kanuni hizi zinazolenga kuikwamua nchi kutokana na madhila yanayotokana na ugonjwa huu.

Katika siku za hivi karibuni, viongozi hao wa kisiasa, kuanzia Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi hadi madiwani katika maeneo ya mashinani, wameonyesha mfano mbaya kwa kuonekana kuendelea na mikutano ya kisiasa.

Kwa mfano, Alhamisi wiki jana, Mkurugenzi Mkuu wa Afya nchini, Dkt Patrick Amoth alijumuika na zaidi ya waombolezaji 400 katika hafla moja ya mazishi katika kijiji cha Kihate, eneobunge la Mukurweini, Kaunti ya Nyeri.

Hapa ni nyumbani kwa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ambaye alikuwa amewakilishwa na Dkt Amoth katika shughuli hiyo.

Isitoshe, waombolezaji hao, waliojumuisha wabunge na madiwani kutoka eneo hilo, walilindwa na kundi kubwa zaidi la maafisa wa usalama. Wanahabari waliofika kunakili matukio walidhulumiwa na maafisa hao pamoja na vijana waliokodiwa, ishara kwamba yaliyokuwa yakiendelea hapo yanaenda kinyume na kanuni za kudhibiti Covid-19.

Waziri Kagwe na Dkt Amoth wanapaswa kuwa kielelezo bora kwa umma kwa kuwa katika mstari wa mbele katika utekelezaji wa kanuni za kupambana Covid-19.

Isiwe kwamba raia wa kawaida ndio wanaokamatwa wakikiuka sheria hizi ilhali maafisa wakuu hawa wa Wizara ya Afya inayohimiza utekelezaji wazo, wanasazwa. Virusi vya corona havijali hadhi ya mtu.

Ikiwa Mwanamfalme wa Uingereza Charles na Waziri Mkuu Boris Johnson walipata homa ya corona sembuse akina Amoth!

Vilevile, ninahisi kuwa Rais Kenyatta, Naibu wake Dkt William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (Cotu-K), Bw Francis Atwoli, miongoni mwa wanasiasa wengine wamekuwa wakionyesha mfano mbaya kuhusiana na utekelezaji wa marufuku ya mikutano ya kisiasa.

Swali langu ni je, kuna haja gani raia wa kawaida kuadhibiwa wakihudhuria mikutano inayoshirikisha zaidi ya watu 15 ilhali Rais Kenyatta na Bw Odinga wanafanya mikutano ya kisiasa yenye zaidi ya wahusika 200?

Juzi, kiongozi wa taifa aliongoza mkutano wa kundi la wabunge wa Jubilee uliohudhuriwa na wabunge 212 katika Ikulu ya Nairobi.

Ingawa inadaiwa kuwa kila mmoja aliketi umbali wa mita moja na nusu na mwezake, hiyo haina maana kuwa hakukuwa na mtagusano wowote kati ya washiriki.

Mikutano kama hii, ya Dkt Ruto katika eneo la Nandi na Bw Atwoli katika Kaunti ya Kajiado, haikufaa wakati huu maambukizi yanapozidi kwa kasi hata kama washiriki walivalia barakoa.

Ninawahimiza viongozi wetu kuwa mbele katika kuheshimu kanuni za kupambana na Covid-19 ili wananchi waige mfano huo.

Kanuni hizi zizingatiwe na viongozi wote wala si raia pekee.

[email protected]