WASONGA: Wabunge wapiganie kurejea kwa bei nafuu

WASONGA: Wabunge wapiganie kurejea kwa bei nafuu

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi na wabunge wameamua kuwachezea shere Wakenya kuhusiana na suala muhimu la bei ya mafuta wakijifanya kuwa watetezi wao.

Lakini ukweli ni kwamba Bw Muturi na wabunge wote 349 ndio wamewasababishia Wakenya madhila yanayowakumba wakati huu kutokana na ongezeko la bei ya mafuta kwa kiwango cha juu kupita kiasi.

Ni unafiki mkubwa kwa Bw Muturi, ambaye ametangaza azma ya kuwania urais 2022, kuamuru Kamati ya Fedha kuchunguza ikiwa kuna sababu nyinginezo zilizochangia hatua hiyo mbali na msururu wa ushuru ambao hutozwa bidhaa za mafuta.

Aidha, ameitaka kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Homa Bay kuandaa mswada wa marekebisho ya sheria za ushuru wa ziada ya thamani (VAT) kukinga bidhaa za mafuta kutokana na ushuru huo.

Bw Muturi aliamuru kamati hiyo kuwasilisha ripoti, na mswada huo bungeni baada ya siku 14 kuanzia Jumanne, Septemba 21, 2021.

Kabla ya Spika kutoa amri hiyo mjadala mkali ulishamiri bungeni huku wabunge wakielekeza ‘mishale’ ya lawama kwa serikali, Rais Uhuru Kenyatta na muafaka kati yake na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Kwa kuwa nyongeza ya kati ya Sh7.5 na Sh12 kwa bei za petroli, dizeli na mafuta taa itaendelea kutekelezwa hadi Oktoba 14, agizo la Bw Muturi kwa wabunge halitawakinga wananchi dhidi ya makali ya bei hizo mpya zilizotangazwa na Mamlaka ya Kusimamia sekta za Kawi na Mafuta (EPRA).

Kamati ya Bi Wanga itakapokuwa ikiwasilisha ripoti yake, na kielelezo cha mswada wa marekebisho ya sheria za ushuru, hapo Oktoba 7, tayari zitakuwa zimesalia siku saba kabla ya Epra kutangaza bei zitakazotumika kati ya Oktoba 14 hadi Novemba 14, 2021.

Isitoshe, hata ingawa Bw Muturi atatumia mamlaka yake kulingana na kanuni za Bunge kufupisha muda wa kushughulikiwa kwa mswada huo wa marekebisho ya sheria hiyo ya VAT, muda huo unaweza tu kupitshwa mapema mwezi Desemba.

Kwa mtazamo wangu, spika huyu na wabunge hawajawasaidia Wakenya kwa njia yoyote kwa hatua waliyochukua ya kuanzisha mchakato wa kuondoa ushuru huo ulioanza kutekelezwa baada ya wao kupitisha Mswada wa Fedha wa 2018.

Kadhalika, tayari kiongozi wa wengi Amos Kimunya na mwenzake wa upande wa wachache John Mbadi wamepinga kuondolewa kwa ushuru wa VAT wa kiwango cha asilimia nane kwa mafuta.

Bw Kimunya, ambaye ni waziri wa zamani wa Fedha, alisema kuondolewa kwa ushuru huo kutavuruga bajeti ya serikali na kuinyima mapato ya kiwango cha Sh35 bilioni kwa mwaka.

Ikizingatiwa kuwa Bw Kimunya ndiye mwakilishi wa Rais Kenyatta na serikali yake bungeni, uwezekano wa bunge kupitisha mswada utakaoandaliwa na kamati ya Bi Wanga ni finyu mno.

Pendekezo langu ni kwamba wabunge washinikize Serikali Kuu irejeshe afueni ya bei ya mafuta ili kudhibiti ongezeko la bei ya bidhaa hizo.

Hii ni kwa sababu mojawapo ya sababu zilizochangia ongezeko la bei ya mafuta kwa kiwango kikubwa mwezi huu, kulingana na Epra, ni kuondolewa kwa nafuu hiyo ya kiwango cha Sh1.4 bilioni.

Pili, wabunge waandae sera ya kuihimiza serikali kuimarisha matumizi ya kawi mbadala kama vile mvuke na jua na upepo katika mahitaji ya kila siku badala ya kutegemea mafuta ambayo bei yake inapanda kila mara katika masoko ya kimataifa.

You can share this post!

DOMO KAYA: Jamani nani kamkula fare?

MATHEKA: Kuongezeka kwa mapinduzi Afrika ni hatari kwa...