Makala

WASONGA: Wanasiasa sasa wapunguze joto la kisiasa kuhusu BBI

November 28th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

ULIKUWA uamuzi wa busara kwa kamati ya kiufundi ya mpango wa maridhiano (BBI) kukubali mabadiliko katika mswada wa marekebisho ya katiba kwa kuondoa mapendekezo ambayo yalikuwa yameibua upinzani kutoka kwa makundi mbalimbali ya wadau.

Kwa mfano, kamati hiyo iliondoa mapendekezo kama vile kubuniwa kwa Baraza la Kitaifa la Polisi (NPC), usemi wa vyama vya kisiasa katika uteuzi wa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na usemi mkubwa wa rais katika uteuzi wa mshikilizi wa afisi ya kupokea malalamishi kuhusu majaji.

Bunge la Seneti pia limeongezewa mamlaka ya kupiga msasa baadhi ya washikilizi wa afisi za kikatiba. Inatarajiwa sasa kwamba, mchakato wa marekebisho ya katiba hautaibua jopo la kisiasa, haswa wakati huu ambapo Wakenya wanazongwa na changamoto nyingi za kiuchumi zilisosababishwa na janga la corona.

Nafahamu fika kwamba, mswada wa sasa hauwezi kuwaridhisha Wakenya wote hususan pendekezo la kuongezwa kwa idadi ya wabunge na maseneta kutoka 416 hadi zaidi ya 550.

Huenda idadi hiyo ikaongezeka kupitia uteuzi wa wabunge zaidi kuafikia hitaji la usawa wa kijinsia.

Japo Naibu Rais William Ruto angali anasema kuna nafasi ya kupatikana kwa muafaka kuhusiana na masuala tata (ambayo hakuyataja) anapasa kutambua kwamba, hata katiba ya sasa haikuungwa mkono na wapiga kura wote katika kura ya maamuzi ya Agosti 4, 2010.

Katiba hii iliungwa na asilimia 68 pekee ya wapiga kura ya NDIYO huku asilimia 32 wakipiga kura ya LA.

Licha ya pingamizi hizo zilizobuliwa na yuyu huyu Dkt Ruto na viongozi wa kidini, taifa hili limetumia katiba hii kwa mwongo mmoja sasa, japo inasheheni dosari kadha.

Wito wangu kwa wanasiasa wa mirengo ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa upande mmoja na Dkt Ruto kwa upande mwingine ni kwamba, wakome kutumia mchakato wa BBI kuchochea uhasama miongoni mwa Wakenya.

Mikutano ya kupigia debe au kupinga mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia BBI iendeshwe katika kumbi za kijamii huku masharti ya kudhibiti maambukizi ya Covid-19 yakizingatiwa.

Kimsingi, shughuli hii haipaswi kufyonza pesa nyingi za umma wakati huu ambapo janga hilo limewasukuma zaidi ya Wakenya milioni mbili kwenye lindi la umasikini kiasi kwamba, hawawezi kumudu mahitaji yao ya kimsingi kama chakula, kulingana na ripoti ya hivi punde ya Benki ya Dunia (WB).

Kwa mfano, karatasi za kura ya maamuzi zichapishwe nchini.

Bw Odinga naye akome kuchochea hisia za Wakenya kwa kukariri kauli mbiu ya “Nobody Can Stop Reggea” (Hakuna atakayezuia Reggea) ambayo inatoa mwanya kwa mahasidi wake wa kisiasa kuvumisha ufasiri kwamba BBI inalazimishiwa wananchi.