Makala

WASONGA: Wizara itoe fedha kwa shule kulipa wafanyakazi

July 22nd, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

RAFIKI yangu ambaye ni mwalimu mkuu katika shule moja ya upili Kaunti ya Nyandarua, juzi aliniambia kuwa walinzi wawili shuleni mwake wametoweka kwa kukosa mishahara yao ya miezi ya Mei na Juni.

Alisema hali hiyo imechangiwa na kuwa Wizara ya Elimu haijatuma fedha za kufadhili mahitaji ya shule kwa muhula wa pili ilipotangaza kuwa shule zitafunguliwa mwaka ujao.

Hata hivyo mwalimu huyu alisema “amebahatika” kupata usaidizi wa wazee wawili kutoka kijiji kimoja cha karibu na shule ambao wamekubali kuchunga mali ya shule hiyo, kwa kujitolea, kwa matarajio kwamba hivi karibuni serikali itatuma fedha za kuajiri walinzi wengine.

Changamoto kama hizi zinawakumba walimu wakuu wengi wa shule za msingi na upili za umma kwani tangu mwezi Mei, Wizara ya Elimu haijatuma fedha zozote kwa taasisi hizo.

Wizara inasahamu kuwa licha ya kwamba wasimamizi wa shule waliwapa likizo ya lazima walimu vibarua na wafanyakazi wasio walimu, kama vile wapishi, wasimamizi wa mabweni, madereva na makutubu, huduma za baadhi ya makarani bado zinahitajika.

Wale vibarua wa kutunza mazingira kwa kufyeka nyasi pia bado wanastahili kulipwa ujira wao.Isitoshe, walimu wakuu bado wanapaswa kulipa ada za mahitaji ya kimsingi shule kama vile umeme na maji.

Hizi ni gharama ambazo shule huweka kwenye bajeti zao kuanzia Januari kwa matarajio kwamba zitalipwa kutokana na fedha ambazo hutolewa na serikali chini ya mpango wa elimu bila malipo.

MAHITAJI MUHIMU

Kwa kukosa kutoa fedha za muhula wa pili ambazo zilipaswa kugharamia mahitaji ya kimsingi kama ya mabawabu, serikali inawaweka walimu wakuu katika hali ngumu.

Hii ina maana kuwa kuna hatari ya mali ya shule kuibiwa ikiwa serikali haitaitikia ombi la walimu wakuu kwamba itume angalau sehemu ya fedha za muhula wa pili.

Kando na hayo, serikali inapasa kutuma fedha za miradi ya maendeleo ili walimu wakuu waweze kuzitumia kuweka maandalizi ya kuafiki kanuni za kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona shule zitakapofunguliwa mwaka ujao.

Wizara ya Elimu ilipotangaza kuwa kalenda ya masomo ya mwaka huu imefutiliwa mbali, shule zilitarajiwa kutumia muda wa miezi sita kuweka mikakati ya kuafiki kanuni za Wizara ya Afya za kupambana na janga hili.

Kwa mfano, wasimamizi wa shule ambazo hazina vianzo vya maji vya kutegemewa, watahitaji fedha za kugharamia uchimbaji wa visima au ununuzi wa tangi za maji ili wanafunzi watakaporejea kuwe na maji ya kutosha ili kuwawezesha kunawa mikono nyakati zote.

Pia walimu wakuu wanahitaji fedha za kununua sanitaiza na vipima joto na kununua dawa za kuangamiza viini ikizangatiwa kuwa baadhi ya shule za upili zinatumiwa kama vituo vya karantini.

Inavunja moyo kwamba kwa kujivuta kufadhili maandalizi kama haya, serikali itakuwa ikihatarisha maisha ya wanafunzi shule zitakapofunguliwa.