Wataalam waanza kusaka kiini cha corona jijini Wuhan

Wataalam waanza kusaka kiini cha corona jijini Wuhan

Na AFP

WUHAN, China

KUNDI la wataalamu 10 kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), limeanza kufanya utafiti kuhusu kiini cha virusi vya corona jijini Wuhan baada ya kumaliza muda wa siku 14 kwenye karantini Alhamisi.

Wataalamu hao wa masuala ya utafiti wa afya walifika China Januari 14 na utafiti wao utajikita katika jiji la Wuhan ambako kisa cha kwanza cha corona kiliripotiwa Desemba 2019.

Amerika na mataifa mbalimbali duniani yatakuwa yakifuatilia shughuli za wataalamu hao ili kufahamu ukweli kuhusu virusi hivyo vilivyoua zaidi ya watu milioni mbili kote ulimwenguni. Virusi hivyo pia vilivuruga maisha ya wengi na uchumi wa nchi kadhaa duniani.

Hata hivyo, haikufahamika ni lini na wapi ambako wataalamu hao wataanzia utafiti wao jijini Wuhan kwa kuwa wanashirikiana na serikali ya China ambayo haikutoa habari zozote kuhusu suala hilo.

Imekuwa ikidaiwa kwamba virusi vya corona vilianzia kutoka kwa popo kisha kuenea katika soko la kuuza nyama ya wanyamapori jijini Wuhan.

WHO imekuwa ikisisitiza kwamba itachunguza na kufuatilia utafiti huo kwa makini na undani ili kufahamu ukweli.

Utawala wa Rais mpya wa Amerika, Joe Biden pia unaonekana kufuatilia utafiti huo kwa karibu, ukisisitiza kuwa lazima pia ufahamu kiini cha virusi hivyo.

Msemaji wa Ikulu ya White House, Jen Psaki alisema kuwa kumekuwa na habari tofauti ambazo zinakinzana kuhusu corona na wakati umefika ulimwengu ujue ukweli.

“Ni vyema ukweli ufahamike ili kuondoa dhana ama habari za uongo. Tunatarajia utafiti wa ndani ambao mwishowe utakuwa na majibu ya kuridhisha kuhusu janga hili la corona,” akasema Psaki.

China imekuwa ikitatiza wataalamu hao wa WHO kufanya utafiti wao na kufikia jana haikuwa imebainika iwapo wataruhusiwa jijini Wuhan na kwa muda gani. Pia ni vigumu kujua aina ya ushahidi ambao umesalia jijini humo ikizingatiwa kwamba virusi hivyo viliripotiwa kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya mwaka moja uliopita.

China imekuwa ikilaumiwa kwamba inaficha ukweli kuhusu corona na ilihusika katika kuviunda virusi hivyo, jambo ambalo utawala wa Beijing umekuwa ukikanusha kila mara.

Aliyekuwa Rais wa Amerika, Donald Trump aliibuka na wazo jingine akiwa mamlakani, akisema watafiti kutoka China walikuwa wakidadavua mengi kuhusu virusi hivyo kwenye maabara kisha vikachipuka na kuanza kuenea.

Waathiriwa na familia zilizopoteza jamaa zao kutokana na corona nao wameshutumu China kwa kuwadhibiti na kuwafuatilia tangu wataalamu wa WHO wawasili nchini humo.

“Hii inaonyesha kwamba kuna jambo la siri ambalo serikali inajaribu kuficha. Wanahofia kwamba familia za wahanga zitazungumza na kutoa habari kwa wataalamu wa WHO,” akasema Zang’ Hi mwenye umri wa miaka 51 ambaye babake aliaga dunia kutokana na corona.

Kulingana na takwimu rasmi kutoka serikali ya China, watu 3,900 walifariki kutokana na corona Wuhan huku idadi ya jumla ya waliokufa nchini humo ikiwa 4,637.

You can share this post!

Joho amruka Kingi kuhusu kugura ODM

Marudio ya uchaguzi wa viongozi wa muungano wa tuktuk na...