Wataalam wakongamana JKUAT kubadilishana mawazo kuhusu kilimo na teknolojia

Wataalam wakongamana JKUAT kubadilishana mawazo kuhusu kilimo na teknolojia

NA LAWRENCE ONGARO

WATAALAM wa kilimo cha kutegemea teknolojia na ubunifu kutoka mataifa tofauti walikongamana katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), Juja wiki jana kujadili maswala ya ubunifu.

Mbali na Wakenya, kongamano hilo lilijumuisha wataalam kutoka mataifa kama Uganda, Ghana, Mali, Zimbabwe, na hata Malawi, ambao walikuwa na maswala mengi ya kujadili kuhusu kilimo.

Mtaalam kutoka Ghana, Kate Obaayaa Sagoe, aliyeandamana na wenzake watano, aliwasilisha mtambo wa kisasa wa kiteknolojia wa kuhifadhi vyakula.

Kulingana na mtaalam huyo, wa masuala ya teknolojia na kilimo, mtambo huo unatumia umeme chapa solar.

Sagoe alisema mtambo huo bado unafanyiwa majaribio kabambe kabla ya kuanza kuuzwa katika masoko ya kimataifa.

“Tumebuni mtambo huu kuwapa motisha wakulima wanaoangazia maswala ya kilimo waweze pia kutumia mtambo huu kuhifadhi mazao yao,” alifafanua mtaalam huyo.

Alisema tayari wanatafuta soko katika mataifa mengine ili raia watumie mitambo hiyo.

Meneja wa Mawasiliano katika Taasisi ya Uanamajumui ya Sayansi za Kimsingi, Teknolojia na Ubunifu (PAUSTI) Bi Faith Mercy Wambui, alisema wataalam hao kutoka mataifa tofauti wako katika chuo kikuu cha JKUAT kwa muda wa mwaka mmoja wakifanya utafiti wa kina kuhusu masomo yanayohusiana hasa na kilimo cha mazao tofauti na teknolojia.

Meneja wa Mawasiliano katika Taasisi ya Uanamajumui ya Sayansi za Kimsingi, Teknolojia na Ubunifu (PAUSTI) Bi Faith Mercy Wambui. PICHA | LAWRENCE ONGARO

“Wataalam hao wanakongamana katika chuo hiki huku wakitoka mataifa tofauti wakibadilishana mawazo. Hatua hiyo inaongeza matumaini ya kujiendeleza zaidi,” alifafanua meneja huyo.

Mtaalam wa kilimo anayesomea uzamifu kuhusu viazi vya kizungu, Bw George Oluoch, alisema wakulima wanafaa kuelewa madhara yanayopatikana kwa zao hilo.

Alisema iwapo wakulima watapata kuelewa jinsi ya kutambua magonjwa yanayoingilia zao hilo bila shaka kutakuwa na mazao ya kutosha kwenye mashamba yao.

Bw Oluoch alisema hivi majuzi alipozuru nchini Malawi kuhudhuria kongamano la kilimo alinufaika kwa kupata mafunzo tosha yanayoweza kuwafaa wakulima.

Alisema baada ya kukamilisha utafiti wake katika uzamifu, atakuwa na nafasi nzuri ya kuwapa wakulima mafunzo na ujuzi zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Mhariri asukumwa ndani kwa kudharau mahakama

UFUGAJI: Bidii yake inavyomvunia utamu wa asali Makueni

T L