Habari za Kaunti

Wataalamu Nyandarua wahimizwa kurejea nyumbani ili ‘kuokoa jahazi’

January 16th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

KUMEIBUKA hofu katika Kaunti ya Nyandarua, kwamba baadhi ya wakazi wake wanaofanikiwa wanapoondoka katika kaunti hiyo, huwa hawarudi tena.

Wengi huwa wanapotelea katika maeneo ya mbali na kuelekeza mafanikio na raslimali zao huko.

Uhalisia huo ndio umemfanya Gavana Ndirangu Badilisha kuwarai wanataaluma kuhakikisha  kuwa hawaelekezi maarifa yao katika maeneo hayo pekee, bali “wamerejea nyumbani kuwafaidi wenyeji”.

Gavana huyo alitoa kauli hiyo Jumatatu, alipokuwa akihutubu katika eneobunge la Kipipiri, wakati wa hafla ya kutoa misaada ya vifaa vya kimasomo kwa wanafunzi wanaotoka katika familia maskini.

“Lazima tufahamu kuwa huwezi kutoroka nyumbani, hata ukienda mbali, kwani mwishowe utarejea huko. Hivyo, wito wetu kwa wanataaluma wetu wanaohudumu katika maeneo tofauti nchini na duniani kote ni kurejea katika kaunti hii na kutoa mchango wao, hasa katika seka ya elimu,” akasema Bw Badilisha.

Gavana huyo alisema kuwa elimu ndiyo njia ya pekee ya kuisaidia kaunti hiyo “kupata mafanikio yanayolingana na mwelekeo wa sasa duniani.”

“Tumejaaliwa kuwa na wanataaluma wengi kama madaktari, wahandisi, walimu, wahadhiri kati ya wengine. Utaalamu wao unaweza kutusaidia sana ikiwa wanaweza kuuelekeza huku,” akasema kiongozi huyo.

Hafla hiyo ilikuwa imeandaliwa na mbunge Wanjiku Muhia anayeliwakilisha eneobunge hilo.

Baadhi ya vifaa vilivyotolewa kwa wanafunzi ni vitabu na madawati.